24.4 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Katibu wa CCM awaweka mtegoni wabunge watano

DAMIAN MASYENENE  – SHINYANGA

BAADHI ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wenyeviti wa halmashauri za Mkoa wa Shinyanga, wametakiwa kuandika barua kueleza kwanini hawakuudhuria kikao cha halmashauri kuu ya chama hicho kilichokuwa kikipokea taarifa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015-2020.

Kikao hicho kilifanyika juzi kwenye ukumbi wa CCM Mkoa wa Shinyanga, ambapo pamoja na wajumbe wengine kilihudhuriwa pia na  Mkuu wa Mkoa huo, Zainab Telack.

Wabunge ambao hawakuudhuria bila kutoa taarifa na majimbo yao kwenye mabano ni Ahmed Salum (Solwa), Steven Masele (Shinyanga Mjini), Jumanne Kishimba (Kahama Mjini), Selemani Nchambi (Kishapu) na Lucy Maenga wa Viti maalum.

Wabunge waliohudhuria na majimbo yao kwenye mabano ni Elias Kwandikwa (Ushetu) Ezekiel Maige (Msalala) na Azza Hilal Mbunge wa Viti Maalum.

Pia kikao hicho kilihudhuriwa ni mwenyekiti mmoja tu wa halmashauri ambaye ni Ngassa Mboje wa Wilaya ya Shinyanga.

Kutokana na hali hiyo, Katibu wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Donald Magesa, alionyesha kukasirishwa na jambo hilo akisema kikao kilipaswa kuhudhuriwa na wajumbe 52 wa halmashauri kuu lakini ni 30 pekee waliojitokeza.

Magesa aliagiza wabunge na wenyeviti wa halmashauri ambao hawakuhudhuria waandike barua kwenda kwa makatibu wa wilaya na zimfikie.

“Naomba kila mwenyekiti wa halmashauri aniandikie barua kwanini hajafika kwasababu hapa anaonekana Ngassa Mboje Mwenyekiti wa Wilaya ya Shinyanga peke yake, wengine wako wapi? Sisi ndiyo tunateua madiwani kwahiyo msiwapende sana madiwani wakawakwamisha.

“Kwa kutumia nafasi niliyonayo tena kama Mkurugenzi wa uchaguzi wa mkoa huu, naomba wabunge ambao hawajahudhuria waandike barua za maandishi wajieleze kwanini hawapo, wasipojieleza tutaweka kumbukumbu na ikifika muda tutapitia mafaili kwahiyo wajiandae,” alisema.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ilani ya CCM kwa kipindi cha Januari 2016 hadi Desemba 2019, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack alisema hatua mbalimbali zimepigwa katika sekta ya kilimo, viwanda, afya, elimu, maji, mifugo na uvuvi.

Alisema kwa kipindi hicho jumla ya viwanja 189 vimejengwa ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Serikali juu ya uanzishwaji wa viwanda vipya, huku Amcos 204, Saccoss 177 na vyama vingine 23 vya ushirika vikifufuliwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles