AVELINE KITOMARY Na AMON MTEGA -DAR ES SALAAM /SONGEA
SERIKALI imetoa wito kwa wananchi kuteketeza barakoa zao baada ya kumaliza matumizi yake kisha kuzitupa sehemu salama, huku ikitoa mwongozo kwa zile za vitambaa ambazo kwa sasa zinatumiwa na watu wengi kujikinga na virusi vya corona.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkuu wa Kitengo cha Maji na Usafi wa Mazingira, Wizara ya Afya, Anyitike Mwakitalima, alisema ni vyema wananchi kufanya hivyo ili kutunza mazingira pia.
“Wale ambao mmevaa barakoa (mask) zile ambazo zinatakiwa kutupwa baada ya kutumika (disposable mask), ukumbuke kabla hujaitupa uitoboe ili mtu mwingine asiokote na kuisafisha na kuirudisha katika mzunguko.
“Kwa baadhi ya nchi zilizopata maambukizi, inasemekana mtu mmoja aliyeambukizwa virusi hivi ana uwezo wa kuambukiza hadi watu 10 kwa wakati mmoja,” alisema Anyitike.
Aidha, alisema kwa wale ambao wanatumia barakoa za kitambaa wahakikishe wanazibadilisha kila baada ya masaa manne ili kuepusha kupata magonjwa mengine.
Alisema ni muhimu kabla ya kuvaa barakoa za vitambaa kwanza zifuliwe kwa maji na sabuni kisha zipigwe pasi ili kujiweka salama zaidi dhidi ya magonjwa.
“Barakoa za vitambaa zinatakiwa zivuliwe kila baada ya masaa manne hadi sita na hakikisha unaifua kwa maji na sabuni, umeinyoosha ili kama kuna virusi humo waweze kufa, usivae barakoa ambazo ni chafu,” alisema Anyitike.
Naye Balozi wa kampeni ya ‘Mikono safi, Tanzania salama’, msanii Mrisho Mpoto (Mjomba), aliwakumbusha Watanzania kuepuka msongamano katika maeneo yote, huku akisisitiza kuwa kama hakuna sababu ya kutoka nje ni vema watulie majumbani.
ZANZIBAR YATANGAZA WAGONJWA WAPYA
Katika hatua nyingine, wakati idadi ya watu wanaopona Covid-19 ikifikia 84 nchini, idadi ya wanaothibitishwa kuwa na virusi hivyo imeongezeka kutoka 299 na kufikia 306.
Takwimu hizo zimeongezeka mara baada ya jana Waziri wa Afya wa Serikali ya Mpinduzi ya Zanzibar (SMZ), Hamad Rashid Mohamed kutangaza ongezeko la wagonjwa saba wa corona na kufanya idadi ya wagonjwa visiwani humo kufikia 105 kutoka 98.
Akitoa taarifa hiyo, Waziri Hamad alisema wagonjwa wapya wote ni raia wa Tanzania na wakazi wa Unguja.
“Wizara ya Zanzibar inatoa taarifa ya ongezeko la wagonjwa wapya saba wa corona (Covid-19) na kufikia idadi ya wagonjwa 105 kutoka 98 ambao tuliwatolea taarifa siku ya Aprili 24 mwaka huu, wagonjwa wote ni raia wa Tanzania, wanatokea Unguja.
“Wagonjwa 36 wameruhusiwa kwenda nyumbani baada ya dalili zao za maradhi kuondoka, ikiwemo homa, kikohozi, kifua kubana, na kuumwa kichwa.
“Hata hivyo, wagonjwa hao wote wanashauriwa kubaki katika nyumba zao kwa siku 14 na huku wataalamu wetu wa afya wakiendelea kuwafuatilia kwa karibu kabla ya kuruhusiwa kurudi kwenye shughuli zao za kawaida za maisha,” alisema Waziri Hamad.
Aidha aliwataka wananchi ambao wana dalili za kikohozi, homa kali na kupiga chafya kujitokeza katika vituo vya afya au kupiga simu kwa namba 190.
“ Ni vyema mgonjwa mwenye dalili za maradhi haya asijichanganye na wagonjwa au watu wengine, na tuache tabia ya kujitibu wenyewe kwani kwa kufanya hivyo tutaendelea kueneza maambukizi na vifo vinavyohusiana na ugonjwa huo,” alisisitiza.
Hamad aliendelea kuwasisitiza wananchi kuchukua tahadhari zote za kujikinga na ugonjwa huo zinazotolewa mara kwa mara na wataalamu wa afya.
“Tahadhari hizo ikiwemo kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni, kuepuka misongamano hasa katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani na kuahirisha safari za nje na ndani ya nchi zisizo za lazima.
“Pia vyombo vya habari vinahimizwa kupata taarifa za ugonjwa huo wa Covid-19 kutoka Wizara ya Afya, wananchi waendelee kumwomba Mwenyezi Mungu azidi kutulinda na kutuepusha na maradhi haya,” alisema Waziri Hamad.
Mwishoni mwa wiki hii, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema wagonjwa 108 waliothibitishwa na virusi hivyo hawaonyeshi dalili zozote huku kati ya hao 37 wakithibitishwa kupona na kuruhusiwa.
MBARONI AKIDAIWA KUSEMA DAWA YA CORONA NI KUNYWA PILIPILI KICHAA, KUJIPAKA UPUPU
Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma, linamshikilia mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Ibrahimu Bukuku (26) kwa tuhuma za kusambaza ujumbe kwenye mitandao ya kijamii, akisema dawa ya corona ni kunywa pilipili kichaa na kujipaka upupu.
Akizungumza ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Simon Maigwa, alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa katika Kijiji cha Lunyele, Kata ya Tingi, Wilaya ya Nyasa mkoani humo.
Kamanda Maigwa alidai kuwa mtuhumiwa ambaye ni mwanafunzi wa shahada ya sayansi fani ya biolojia, alisambaza ujumbe huo kupitia simu yake ya kiganjani.
Alisema katika ujumbe huo ambao ulisambazwa kwenye makundi ya Whatssap, mtuhumiwa alidai kuwa dawa ya virusi hivyo ni kuchukua pilipili kichaa sufuria moja iliyotwangwa, kuchanganya na maji vikombe vitano kisha kunywa kutwa mara saba kwa siku tatu.
Alidai mtuhumiwa huyo kwenye ujumbe wake alisema mtu akishakunywa pilipili hizo, siku ya nne achume upupu na kujipaka mwili mzima.
Alisema jambo hilo ni upotoshwaji mbele za jamii na linachukuliwa mchezo kwenye gonjwa hili la Covid-19.
Kamanda Maigwa alisema kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kuwatafuta wale wote wanaofanya mchezo na ugonjwa huu wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria kujibu mashtaka yanayowakabili.