26.5 C
Dar es Salaam
Friday, September 24, 2021

Wabunge watoana jasho wakibishania maji

 RAMADHAN HASSAN -DODOMA

MBUNGE wa Chemba, Juma Nkamia (CCM) na Kunti Majala wa Viti Maalumu (Chadema), wote wakitokea Chemba mkoani Dodoma, wametoana jasho bungeni wakibishania shida ya maji katika jimbo hilo,.

Kunti jana alipata nafasi ya kuchangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Maji kwa mwaka 2020-2021 ambapo wakati akichangia mara kwa mara alisimama Nkamia na kumpa taarifa.

Kunti alidai Jimbo la Chemba kuna shida ya maji, lakini wizara haijafanya lolote kuwasaidia wakazi wa jimbo hilo na kwamba wananchi wamekuwa wakinywa maji na mbwa, tembo na fisi.

“Ni ni sisi tu Tanzania ambao bado tunakunywa maji na mbwa, tembo na fisi, ni sisi Watanzania nchi iliyojaaliwa, nchi yenye maziwa na maporomoko bado tuna kunywa maji machafu.

“Kaka yangu (Makame Mbarawa) mimi nasikitika sana sijui unamdanganya nani, sisi Chemba vijijini 66 havina maji,” alisema Kunti.

Wakati akiendelea kuchangia, alikatishwa na Mbunge wa Kilolo, Venace Mwamoto (CCM) ambaye alimpata taarifa akimtaka aache kutumia maneno makali kwamba watu wanakunywa maji na mbwa.

“Namuomba mdogo wangu aache kutumia maneno makali, kwamba wanakunywa maji na mbwa, niombe sana kwa kuwa ni mstaarabu,” alisema Mwamoto.

Akichombeza, Spika Job Ndugai alisema; “Mwamoto anaomba suala hili na tunajua anatoka Iringa kule kwenye mbwa.”

Akiendelea kuchangia, Kunti alisema; “najua (Mwamoto) vimate vimemtoka.”

Wakati Kunti akiendelea kuchangia, alisimama Nkamia na kumpa taarifa akisema Watanzania wanakunywa maji na mbwa ni kashfa hata kwa wakazi wa Chemba ambako ndiko anakotoka, hivyo akamwomba mbunge huyo atumie lugha ya staha.

“Nilitaka nimpe taarifa, Chemba asilimia 57 hawana maji, ukisema Watanzania wanakunywa maji na mbwa hii ni kashfa kubwa kwa wananchi wa Chemba, ningemuomba atumie lugha ya staha na ajue anazungumza na watu wa aina gani,” alisema Nkamia.

Akiendelea kuchangia, Kunti alisema anamshukuru Nkamia kwa kutambua kwamba zaidi ya asilimia 57 ya wakazi wa Chemba hawana maji.

Kunti alisema baadhi ya vijiji katika Jimbo la Chemba kikiwemo Kijiji cha Churuku wamesubiria kuchimbiwa visima, lakini wamesubiri kwa zaidi ya miezi tisa hakuna jibu lolote.

“Ni zaidi ya miezi tisa hakuna maji, wananchi wanasubiri hawaelewi hatma, unapokuwa unakuja nitaomba uwaeleze Watanzania lini vijiji hivi vitapewa maji,” alisema Kunti.

Wakati akiendelea kuchangia, alikatishwa na Nkamia ambaye alimpa taarifa kwamba kuna baadhi ya visima vina matatizo, lakini Serikali imevifanyia ukarabati.

“Manantu kuna kisima cha maji kimetumika, hata mimi nimekikuta kina matatizo ya mindombinu, Birise kuna matatizo, Handa kuna kisima cha muda mrefu kwa sababu kuna madini ya uraniam, hivyo Kunti asiseme hivyo,” alisema Nkamia.

Spika Ndugai aliingilia kati na kumwambia Kunti asilete maneno ya uongo bungeni.

Akiendelea kuchangia, Kunti alisema anamshukuru Nkamia kwa kusema ukweli kwamba kuna visima na maeneo ambayo hayana maji katika Jimbo la Chemba. 

Kunti alisema anamshangaa Waziri wa Maji kuleta takwimu za uongo bungeni kwamba vijijini maji yanapatikana kwa asilimia 70 na mijini asilimia 80.

“Takwimu hizo tuna miradi 652 Ruwasa ilipanga kutekeleza, imetekeleza 94 tu, naomba nikuulize asilimia 70 ya upatikanaji wa maji vijijini umeipata wapi?” alihoji mbunge huyo.

Katika hatua nyingine, Mbunge wa Viti Maalumu, Rhoda Kunchela (Chadema) alisema amekuwa akipiga kelele kuhusu ukamilishwaji wa miradi ya maji katika Jimbo la Mpanda, lakini wizara imeshindwa kutekeleza.

“Niombe miradi iliyokwama imaliziwe, tunahitaji maji kwa ajili ya kuendeleza miradi yetu ya umwagiliaji. Uhitaji wa maji tunahitaji lita 10,000 lakini tunapata 4,000 na tuna wakazi zaidi ya 200,000 niombe Serikali ikamilishe miradi mbalimbali.

 “Kuna miradi ambayo imesimama kwa muda mrefu, tuna Milala, Kamkulu, Ilembo na maeneo mengine. Wananchi Katavi wanapata tabu, hata barabara za lami hatuna,” alisema Kunchela.

Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya (CUF) aliomba Serikali kila siku iwe inatoa mwendelezo wa taarifa za ugonjwa wa corona huku akitaka usafiri wa umma uangaliwe kwani hakuna tahadhari yoyote inayochukuliwa.

“Naomba tuangalie suala la usafiri wa ‘public’, naomba jambo hilo liangaliwe, Serikali itoe fedha za kutosha katika corona, ikiwezekana tupunguze fedha katika miradi mikubwa ili fedha ziende huko,” alisema Sakaya. 

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
157,854FollowersFollow
518,000SubscribersSubscribe

Latest Articles