25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mwenzenu simwelewi Profesa Lipumba

lipumbaNa EMELESIANA JOHN (OUT)

MWAKA jana wakati mbio za Uchaguzi Mkuu zikiwa zimenoga, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alitangaza kujiuzulu nafasi hiyo.

Alipojiuzulu Watanzania wengi, mimi nikiwa miongoni mwao, nilishtushwa na uamuzi huo kwa sababu Profesa Lipumba ambaye ni msomi anayeheshimika ndani na nje ya nchi, alikuwa akihitajika zaidi na viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) pamoja na chama chake kwa ujumla.

Profesa Lipumba ni msomi wa hadhi ya dunia, ni mwanasiasa mwenye uwezo mkubwa wa kushawishi na kuaminiwa na pia ni mzee mwenye umri wa kuheshimiwa na watu wengine aliowazidi umri na wanaomzidi.

Kwa maana hiyo, anapofanya jambo unaloona haliendani na usomi na umri wake, lazima ujiulize mara mbili mbili ili kujua ni kwanini amefanya jambo hilo.

Nayasema haya kwa sababu wakati anajiondoa CUF na kuelekea nje ya nchi, wafuasi wa vyama vya upinzani ambao walikuwa wakiwahimiza wananchi kuhitaji mabadiliko, walikuwa wakiamini mchango wa mawazo wa mwanasiasa huyo ulikuwa muhimu katika harakati za kukiondoa madarakani Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Pamoja na matumaini hayo waliyokuwa nayo baadhi ya Watanzania, msomi huyo pamoja na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, waliamua kukaa pembeni katika kipindi walichokuwa wakihitajika zaidi.

Hayo yalitokea na waliobaki katika vyama vya siasa vya upinzani, hawakuyajali na badala yake walitulia na kukusanya nguvu upya ili kuikabili CCM wakati wa uchaguzi huo mkuu uliokuwa na msisimko wa aina yake.

Binafsi niliamini baada ya Profesa Lipumba kuachia ngazi, hatarudi tena katika chama hicho na kutaka aendelee kushika wadhifa wake huo na badala yake niliamini angeendelea kuwa mwanachama wa kawaida kama alivyosema wakati anatangaza kung’atuka katika wadhifa wake huo.

Pamoja na fikra hizo ambazo naamini baadhi ya Watanzania walikuwa nazo, hivi karibuni Profesa Lipumba ambaye ni kati ya wanasiasa wanaoheshimika zaidi nchini, alitangaza kutaka kurejea katika nafasi yake na kueleza jinsi Katiba ya chama chao inavyomtambua.

Sipingani na msimamo huo lakini sielewi kwanini alijiuzulu na sielewi kwanini sasa anataka tena awe mwenyekiti wa chama alichokiacha katika kipindi alichokuwa akitakiwa.

Simwelewi na naamini itanichukua muda kidogo kumwelewa kwa sababu hata nguvu anayotumia kuingia tena madarakani ni kubwa na inaonekana kuungwa mkono na baadhi ya vyombo vyetu vya ulinzi.

Ni nguvu kubwa inayotumika kwani hata yeye anaposimama katika vyombo vya dola kutetea uamuzi wake, anaongea kwa kujiamini utadhani hawajawahi kukiacha chama katika mazingira aliyokuwa akihitajika.

Pamoja na hayo, namtakia kheri mwanasiasa huyo katika harakati hizo ila nazidi kumsisitiza aueleze umma kwamba, wakati anajiondoa madarakani, alishawishiwa na kitu gani na kitu gani kimemshawishi arudi tena madarakani ingawa ameonekana kukigawa chama chake.

Hata hivyo, nawatahadharisha CUF, wawe makini katika kukabiliana na mwenzao huyo kwani bila kufanya hivyo, wanaweza kukisambaratisha chama chao badala ya kukijenga kama ambavyo wamekuwa wakisisitiza katika majukwaa ya siasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles