OMARY MLEKWA Na SAFINA SARWATT-HAI
WATU wasiofahamika wamechoma nyumba ya Mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Hai, Mkoa wa Kilimanjaro, Dk. Amini Uronu.
Nyumba hiyo iliyoko Kijiji cha Nshala, Kata ya Machame Mashariki, ilichomwa moto usiku wa kuamkia juzi saa sita usiku, baada ya watu hao kuimiminia petroli.
Wakati wa tukio hilo, kiongozi huyo wa CCM alikuwa amelala ndani na familia yake ya watu saba. Moto huo ulimjeruhi Dk. Uronu miguuni na mikononi.
Akisimulia tukio hilo, mtoto wa Dk. Uronu, Zahadi Uronu, alisema wavamizi hao waliwasha moto kupitia katika milango miwili ya nyumba hiyo.
“Tulishtuka baada ya kuona moto ukiwaka katika milango yote miwili. Kwa hiyo, tulianza kupiga kelele za kuomba msaada na ndipo watu walifika na kuvunja mlango wa nyuma na hatimaye tulitoka wakati huo moto ulikuwa mkubwa na
tayari baba alikuwa amejeruhiwa miguuni na mikononi.
“Huu moto utakuwa umewashwa na watu kwani kwa upande wa nyuma, ulianzia kwenye mlango wa jikoni na mlango wa mbele ulianza kuchoma vitu vilivyokuwa barazani.
“Wakati moto unawaka, ndani tulikuwamo watu wanane na kati ya hao, baba ndiye amejeruhiwa ila mama yetu alipoteza fahamu kutokana na mshtuko,” alisema mtoto huyo.
Naye mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Cuthbeth Uronu, alisema alikwenda eneo la tukio baada ya kusikia Dk. Uronu na familia yake wakipiga kelele za kuomba msaada.
“Nilifika hapa usiku na nilikuta moto ukiwaka milangoni ambapo nilishirikiana na wenzangu kuvunja mlango wa nyuma kwa kutumia gogo lililokuwa
hapo nje na kufanikiwa kuwatoa watu waliokuwa ndani,” alisema.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Hai, Gellasius
Byakanwa, aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili
kuwabaini waliohusika na tukio hilo.
“Najua wananchi mmeonyesha ushirikiano wa kutosha katika kunusuru maisha ya familia hii, lakini naombeni mtoe ushirikiano huo huo wakati wa kuwatafuta wahusika wa moto huo,” alisema Byakanwa.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kilimanjaro, Selemani Issa, alithibisha kutokea kwa
tukio hilo na kusema mwenyekiti huyo wa CCM amelazwa katika Hospitali ya St Joseph ya mjini Moshi.