33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mwalimu angekuwa hai angejiunga Chadema

edwin-mtei-na-edward-lowassaNa Edwin Mtei, Arusha

NILIMFAHAMU Mwalimu Nyerere nikiwa mwanafunzi wa Tabora High School mwaka 1951-52, baada ya Mwalimu kuwa amerudi kutoka Ulaya. Lakini tulikuja kufahamiana zaidi na Mwalimu baada ya kuwa nimeanza kazi serikalini mwaka 1959 ambapo nilikwenda Dar es Salaam na kukutana na rafiki yangu tuliyekuwa naye Makerere, Uganda akiitwa Mwanjisi.

Sasa huyu Bwana Mwanjisi alikuwa Katibu pale TANU na nilipoingia mwaka huo ndiye aliyenipeleka kwa Mwalimu Nyerere pale nyumbani kwake Magomeni, tukafahamiana kwa mara ya pili tena.

Tukiwa pale Mwalimu aliniambia tufanye kazi na tujifunze kutoka kwa walowezi waliokuwa wakikaribia kuondoka, ili tuweze kuongoza nchi na kuchukua Serikali. Nilimwambia sawa Mwalimu.

Kutokana na mazingira ya wakati huo karibu wafanyakazi wa Serikali tulijikuta tumejenga utaratibu wa kula chakula cha mchana sehemu moja katikati ya Jiji la Dar es Salaam na wakati mwingine tulikutana na Mwalimu naye akija kula chakula hapo hapo.

Baada ya hapo nilikwenda nchini Kenya kikazi na nikiwa huko, Mwalimu aliamua tena kunirejesha nyumbani kisha nikateuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha. Na kuanzia hapo ndipo nikawa nimeingia kwenye masuala ya uchumi na fedha.

Mwaka 1965, baada ya Mwalimu kuchukizwa na kitendo cha kutopatikana kwa Shirikisho la Afrika Mashariki, kutokana na Jomo Kenyatta kupiga chenga kidogo, Mwalimu alikata tamaa ya kuwa na Sarafu moja ya Afrika Mashariki.

Basi wakati huo mimi nikiwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Mwalimu Nyerere aliniteua nianzishe Benki Kuu ya Tanzania (BOT), ndipo pia nilipoteuliwa kuwa Gavana wa Benki Kuu.

Mwishoni Mwalimu tena aliniteua nikajikuta nimerudi tena East African Community nikaenda kuwa Katibu Mkuu na baada yangu ndipo Charles Nyirabu alipochukua nafasi yangu.

Nikiwa Katibu Mkuu, bahati mbaya kutokuelewana kati ya Kenyatta na Mwalimu mambo yalianza tena kuvurugika. Lakini nakumbuka Jumuiya ilivunjika hasa wakati ule tukiwa tunasherehekea miaka 10 ya Azimio la Arusha na wakati huo huo tukijiandaa kwenda kwenye sherehe za Muungano na kuzinduliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Nakumbuka kule nchini Kenya walifanya matatizo kwa kutoruhusu zile ndege za EAC ziwapeleke wageni waliokuwa wanatakiwa kuhudhuria sherehe hapa Arusha na baada ya hapo ziwapeleke wageni hao visiwani Zanzibar kwa ajili ya kuzindua CCM.

Kwa kweli hatua hiyo ilimkasirisha sana Mwalimu Nyerere na aliamua kufunga mpaka wa Tanzania na Kenya na hapo Jumuiya ikavurugika na kufa. Lakini nilipokuwa najaribu kumuelezea Mwalimu alegeze mambo ili Jumuiya isivunjike kabisa, nilikwenda Nairobi na kufanya mazungumzo na watu wa kule.

Nikiwa huko nilikutana na Katibu wa Kenyatta akanieleza Mzee alikuwa Mombasa hivyo asingeweza kuzungumza naye kwa wakati huo kuhusu mambo yetu kwani tulikuwa tunafanya mambo hovyo hovyo.  Basi baada ya kutoka Nairobi nilirudi Arusha nikaenda tena Dar es Salaam kwani Mwalimu alikuwa ameniita nikiwa huko ndipo tena akaniteua kuwa Waziri wa Fedha.

Nikiwa kwenye nafasi hiyo kumbuka tayari Jumuiya ilikuwa imeshakufa, lakini nikiwa Waziri hapo hapo niliteuliwa kuwa kwenye timu ya Watanzania waliokuwa wakiendesha majadiliano kati ya Uganda na Kenya na Tanzania jinsi ya kugawa mali za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Sasa basi kutokana na kuvunjika kwa EAC na vile vita vya Idd Amin uchumi wetu ulivurugika kabisa na kusababisha kukosa fedha za kigeni hapa nchini. Utakumbuka nikiwa Waziri wa Fedha tayari nilishatembelea nchi za ng’ambo kwa ajili ya kutafuta fedha ili kuhakikisha tunapata fedha za kukabiliana na vita dhidi ya nduli Idd Amin.

Kwasababu thamani yetu ya fedha ilikuwa imekwenda chini sana wakati huo, nililazimika kutafuta fedha ili pia tuweze kufufua uchumi baada ya vita. Kwa kweli nilipata ahadi nyingi kutoka kwa wahisani nje ya nchi ikiwamo Benki ya Dunia kuwa walikuwa tayari kutusaidia bora tu tuhakikishe kwamba tunaimarisha utawala wetu.

Kwani zipo baadhi ya taasisi ambazo zilikuwa zinapewa fedha kutoka BoT na nyingine zilikaribia kufilisika kabisa, hadi pale tulipoamua tena kuwapa fedha za NBC, ambapo walisababisha hata NBC yenyewe kuwa katika wakati mgumu sana kama tusingeingilia.

Kwa hiyo, nilishauri tuimarishe hayo mashirika na taasisi na baadhi tukaribishe watu kutoka nje na ndani kwa ajili ya kuziendesha kwa ubia na Serikali.

Basi watu wa Shirika la Fedha Duniani (IMF) walipokuja nchini walipendekeza mambo ambayo yalimuudhi sana Mwalimu Nyerere na jambo moja lililomuudhi lilikuwa ni kurekebisha thamani ya shilingi.

Kwani wakati huo ilikuwa Dola moja ya Marekani ni sawa na Sh tisa wakati huo. Nakumbuka nilifanya nao mazungumzo na kuwaomba tufike hadi Sh 12. Hapo ndipo Mwalimu alipopaza sauti yake akisema: “Hataweza kupunguza thamani ya shilingi labda mpaka tumuue”.

Sasa hapo hapo ndipo namimi nilipomwambia Mwalimu basi inatosha niamie nakuachia umtafute Mtanzania mwingine atakayekushauri, halafu umteue kuwa Waziri wako wa Fedha. Kwanini mimi siwezi tena kuendelea na kitu ambacho kinaonekana wazi kabisa, kwa hiyo niliamua kuacha kazi mwenyewe.

Na hii ilitokana na watu wasio wataalamu kumshauri Mwalimu vibaya kwamba asikubali kupokea ushauri wangu wakidai IFM ilikuwa inataka kuleta utawala mwingine kwa kumfanya Mwalimu aendeshe nchi kwa sera ambazo haziendani na ujamaa.

Basi baada ya yeye kukataa na mimi nikamwambia nakuachia uchumi wako ujaribu kutafuta mtu atakayeweza kukushauri ili uendeleze uchumi jinsi unavyotaka wewe. Sasa siku najiuzulu, mtu mmoja aliyekuwa anamiliki shamba hili hapa nyumbani kwangu Tengeru alikuwa amefika nyumbani kwangu kule Dar es Salaam akaiona nyumba yangu nzuri sana kule Oysterbay.

Kwa kweli aliipenda nyumba ile na aliomba kuinunua ili watoto wake wakae kule, hivyo nilikubaliana naye nikampa nyumba yangu ya Dar es Salaam na yeye akanipa shamba hili hiyo ilikuwa mwaka 1980.

Mwalimu Nyerere kwa wakati huo angekubaliana na ushauri wangu, tungepata mkopo wa Dola za Marekani milioni 375 kwa ajili ya kuimarisha miundombinu na mashirika yaliyokuwapo na tungekuwa tofauti.

Mwaka 1980 hadi 1986 baada ya Rais Ali Hassan Mwinyi kuchukua madaraka Serikali ilianza kufanyia kazi ushauri ule ule niliowahi kuutoa kwa Mwalimu mwaka 1979.

Alipoingia Rais Mkapa aliendeleza mpango ule ule kwani mashirika ambayo nilitaka yachukuliwe kwa makubaliano badala yake tulikuja kuyauza kwa bei ya bure kabisa kwa watu, hii ni pamoja na Benki ya NBC kupewa bure kabisa kwa makaburu wa Afrika Kusini.

Jambo kubwa ninalotaka kuwaambia leo hii kama Mwalimu angekuwa hai hadi leo, basi angejiunga Chadema nakumbuka katika siku moja ya Sikukuu ya Wafanyakazi iliyofanyika jijini Mbeya, kabla Mwalimu hajaenda kuhutubia wananchi nilikwenda nyumbani kwake na kumpatia Katiba ya Chadema.

Nikiwa pale nakumbuka Mwalimu Nyerere alikisoma kitabu kile kwa muda mfupi tukazungumza na akasifia sana sera za Chadema na kuwaambia Watanzania kuwa Chadema ndio chama kinachoweza kuwa na sera ambazo zinaweza kuokoa nchi hii.

Naamini angeendelea kuwapo leo si ajabu angekuwa mwanachama wa Chadema, angetuimarisha kwani tunatafuta wazee waadilifu katika nchi yetu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles