Na Joseph Lino,
Makampuni matatu ya mawasiliano ya simu nchini yamefanikiwa kutii sheria na kufuata maagizo ya Serikali kuwasilisha maombi ya kuuza sio chini ya asilimia 25 za hisa zao kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam.
Kampuni za Tigo, Vodacom na Airtel zimewasilisha maombi yao ndani ya muda uliotakiwa ilikuingia katika soko la hisa la Dar es Salaam (DSE) kabla ya tarehe ya 31 Desemba kwa mujibu wa mahitaji ya Sheria ya EPOCA na kufungwa Desemba 31 mwaka jana kwa mujibu wa sheria mpya.
Baadhi ya makampuni yakiwamo Smart, Halotel na TTCL bado hazijawasilisha wala kusema chochote kinyume cha maagizo ya lazima yalivyotolewa. Kuna zaidi ya kampuni 96 zilizosajiliwa na Tume ya Mawasiliano (TCRA) na zinafanya shughuli mbalimbali za mawasiliano ili zichunguzwe kisheria kuwa zimewajibika vilivyo kuhusu DSE.
Serikali ilishatangaza TTCL ambayo inaimiliki kwa asilimia 100 itaingia soko la hisa mwaka huu na Airtel ambayo ina asilimia 40 ya umiliki imejipanga na kuomba wakati Halotel ndio kwanza imeingia sokoni na huenda ikasubiri hadi miaka mitatu ipite kama sheria inavyoruhusu lakini hakuna kauli yoyote kutoka Smart ambayo imeonekana kusimamisha hata matangazo yake kwenye vyombo vya habari.
Kwa upande wa Zantel, asilimia 15 ya hisa ni mali ya Serikali ya Zanzibar na ilisajiliwa kisiwani huko.
Mwaka jana serikali ilitoa agizo kwa kampuni za simu kuweka hisa kwenye soko la hisa kupitia sheria iliyopitisha mwezi Juni na Bunge mwaka jana ya lazima inayolenga kuwasaidia wananchi wake kumiliki sehemu ya moja viwanda vya Mawasiliano sekta inayokua kwa kasi zaidi barani Afrika na hapa nchini.
Cha ajabu kuhusu zoezi hilo ni kuwa masharti ya kujiunga ni yaleyale ya hiari kinyume cha watu walivyotegemea, kwani watu walifikiri yatalainishwa ilikuwavutia ila yameimarishwa masharti hayo ili kuongeza uwazi na uwajibikaji kuzuia mwenendo wa makampuni hayo kukosa kutengeneza faida kila mwaka ili kukwepa kodi. Wakionesha kinyume kunahatari ya kuyafuta haswa katika awamu hiyo ya Tano isiyotaka maneno marefu.
Sekta ya mawasiliano ni mmoja ya sekta zinazofanya vizuri nchini huku inazidi kukua kwa kasi ambapo kufikia mwezi Juni mwaka huu watumiaji wa simu walifikia milioni 39.2 huku ikiwa ya pili katika fedha katika benki.
Vodacom ambayo inamiliki asilimia kubwa ya soko la mawasiliano Tanzania inatarajia kupata bilioni 500 wakati itakapoanza kuuza hisa zake.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Vodacom Tanzania ndiyo kampuni kubwa zaidi katika soko la huduma za mawasiliano kwa simu za kiganjani kati ya kampuni saba, ikichukua asilimia 31 ya soko na laini milioni 12.06 hadi kufikia Juni mwaka huu.
Kampuni za Tigo na Airtel zinashikilia nafasi ya pili na ya tatu kwa kuwa na asilimia 29 na 26 ya soko. Kampuni ya Tigo ina laini milioni 11.6, huku kampuni ya Airtel ikiwa na laini milioni 10.3.
Aidha kampuni ya Halotel ambayo ilianza huduma zake mwaka jana imefikisha wateja milioni 2.7, Zantel inahudumia wateja milioni 1.4 na Smart (881.756) na TTCL (304.058).
Wiki iliyopita Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya mawasiliano nchini (TCRA), Eng. James Kilaba alisema huwa makampuni yote ya simu yanayotoa huduma za mawasiliano yalitakiwa kujisajili kwenye soko la hisa la Dar es Salaam (DSE) bila hufanya hivyo yataadhibiwa kwa mujibu wa sheria.
“Nasubiri taarifa kutoka kwenye Mamlaka ya Soko la Mitaji na Dhamana (CMSA)kufahamu idadi ya kampuni ambazo hazijajiorodhesha na adhabu yake kisheria ni kufutiwa leseni ya kutoa huduma,” alisema Kilaba.
Kwa upande mwingine Soko la DSE ilifungua milango kwa wageni kuweza kununua hisa tangu 2011 kutokana kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki lakini Tanzania ni bado inaweka mipaka kwa raia wa kigeni kwa masuala malumu na haswa IPO.
Sheria inasema kuwa wakazi wenye asili ya mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Kenya, Tanzania na Uganda wanapaswa kuwaona wenzao kama raia wa nchini mwao linapokuja suala la fursa za uwekezaji katika nchi zao.
Tanzania inazuia watu wasiokuwa raia kushiriki katika mauzo ya awali kwa umma (IPO) kutokana Serikali ya Tanzania kuweka uwezeshaji kwa wananchi nchini mwake ambao wengi ni wageni katika mambo ya hisa.
Watanzania ni masikini na wengi bado wana mwamko mdogo wa kuzitumia fursa za uwekezaji kupitia masoko ya hisa, mitaji na dhamana, ambapo mpaka sasa kwenye soko la hisa la, DSE wananchi washiriki ni wachache kama ukifananisha na Kenya
Wakenya wameanza kulalamika kuwa wanafungiwa kushiriki katika mauzo hayo yenye neema kubwa ya kiuwekezaji.
Wakati hayo yanendelea TTCL imekanusha habari kuwa yenyewe imeongezewa muda wa kujiunga na Soko la Hisa la Dar es Slaam (DSE) kuwa inafuata miongozo yote ya serikali bila upendeleo na inawajibika kutekeleza sheria bila kisingizio. Taarifa ya Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba, kwa vyombo vya habari kuwa wamechukua hatua kadha ili kukamilisha zoezi la kujiunga na DSE kama Sheria inavyotaka.