NDOA ya mitala si kitu cha ajabu kwa vile inaruhusiwa na moja ya dini kubwa katika dunia huku baadhi ya makabila duniani yakiiruhusu pia.
Kwa sababu hiyo, si kitu cha ajabu kuwa na ndoa hizi za mitaala nchini Afrika Kusini, ambako kabila la Zulu, analotoka Rais Jacob Zuma huiendekeza zaidi.
Zuma mwenyewe ameoa mara sita, licha ya sasa kuwa na wake halali wanne baada ya mmoja kujinyonga na mwingine Nkosazana Dlamini-Zuma, ambaye yuko katika harakati za kumrithi wakiwa wametalikiana June 1989.
Mbali ya wake hao, Zuma ana wanawake kibao wa pembeni wakiwamo aliowalipia mahari, ambao kwa pamoja wamemzalia watoto zaidi ya 20.
Achana na akina Zuma, mfano mwingine ni Mfalme Mswati wa Swaziland, ambaye amekuwa akioa karibu kila mwaka na kumfanya hadi sasa awe na wake 15.
Yote hayo yanaonesha ukawaida wa ndoa za aina hii duniani licha ya baadhi kuwa na mitazamo hasi kuzihusu.
Wakati hali ikiwa hivyo, mfanyabiashara wa mali zisizohamishika nchini Afrika Kusini Musa Mseleku, ambaye ana wake wanne, amejitokeza kujaribu kusafisha ‘hali ya hewa.’
Ni kupitia kipindi kipya cha televisheni kikionesha maisha ya familia yake ya wake wanne na watoto 10.
Lengo kuu ni kutoa elimu kuhusu manufaa ya ndoa za mitala na kufuta dhana hasi zilizoizingira, akieleza pamoja na mambo mengine namna anavyopata msaada mkubwa kutoka kwa wake zake hao.
Mfanyabiashara huyo ambaye pia ameshaandika vitabu kadhaa ikiwamo cha mitala, sambamba wake na watoto wameondokea kuwa nyota wapya wa kipindi hicho kipya kinachoitwaUthando Nes’thembu, ikimaanisha ‘Mapenzi na Mitala.’
Kipindi hicho, ambacho kilianza Mei 19 kimekuwa gumzo katika mitandao ya jamii nchini Afrika Kusini kikifuatiliwa na wengi waliogawanyika kuhusu nafasi ya mila hiyo katika ulimwengu wa kisasa.
Kipindi huangazia maisha ya nyumba yake ya kijijini karibu na Durban, katika pwani ya kusini ya Jimbo la KwaZulu-Natal. Wake wanne kila mmoja ana nyumba yake lakini wanashea ardhi.
"Moja ya mtazamo hasi kuhusu staili ya mitala ni kwamba utamaduni unaolenga kukandamiza wanawake.
“Hiyo ni moja ya sababu kwanini nimeamua kufanya kipindi ili watu waelimike tofauti na wanavyofikiria. Nataka kuwaonesha wanaume kuwa unaweza kuwa katika uhusiano wa mitaala na kuwa mume mwenye kuwajibika," Mseleku anasema.
Hata hivyo, si kila mtu anakubaliana naye, wakati watu kadhaa wakieleza kushukuru kukiona kipindi hicho, baadhi wanaona staili hiyo inaminya uhuru fulani.
Baadhi ya waliochangia wengi wakiwa wanawake walishambulia kile ambacho Mseleku anasisitiza wake zake hutakiwa wawe wamerudi nyumbani ifikapo saa 11.00 jioni.
Pia baadhi hawaonekani kukubaliana na kitendo cha kuomba ruhusa iwapo wote wanne wanataka kwenda kuvinjari na kujimwaga na marafiki zao au kunywa pombe.
Lakini Thobile Mseleku, mke wa tatu katika ndoa hiyo anasema, “Naamini kila mmoja na kila nyumba hasa sisi Waafrika Kusini, tunaamini mume ni kama mungu wako. Hivyo huwezi kufanya kila kitu au uamuzi bila kupata Baraka toka kwa mume."
Musa Mseleku anaongeza kuwa pia naye amewekewa muda wa kurudi nyumbani, saa moja zaidi kabla ya wake zake.
Thobile na Musa wako katika ndoa kwa miaka tisa sasa. Wakati walipokutana, mwanaume alikuwa tayari na wake wawili, na hivyo alijua nini atakacho. Babu na bibi zake pia walikuwa sehemu ya familia ya mitala.
Anasema kwamba wake wanne, wengine wakiwa Busisiwe MaCele, Nokukhanya MaYeni na Mbali MaNgwabe ni kama dada na wanategemeana kwa ushauri na msaada.
Lakini kipindi hicho kinaonesha namna bibi hao wanne wa Mselekus wanavyoweka uwiano wa ratiba zao za kila siku, kikazi ikiwamo biashara na serikalini, kazi za nyumbani na wajibu kama wazazi kwa watoto wao pia kuonesha mivutano ndani ya familia.
Thobile Mseleku anasema: "Chanzo chetu kikuu cha mivutano ni muda. Inaweza kukatisha tamaa iwapo wote tunatoka pamoja huku mmoja akiwa tayari huku ukiwasubiri wengine.”
Naye Musa anaongeza; “Muda ni kitu ninachokifikiria mno. Najaribu kuhakikisha nagawanya muda wangu sawa baina ya wake na watoto wangu kwa usawa bila upendeleo.”
Nchini Afrika Kusini wakati ndoa za mitala zikiwa hazifuatwi na watu wengi, achilia mbali miongoni mwa jamii ya Wazulu..
Ndela Ntshangase, mhadhiri katika shule ya masomo ya Zulu katika Chuo Kikuu cha KwaZulu-Natal, anasema kwamba ndoa za mitaala nchini Afrika Kusini zilianza kufifia katika karne ya 19 wakati wamisionari wa Kizungu waliohubiri kuwa Ukristo unaruhusu ndoa ya mke na mume mmoja tu.
Hivyo basi, kwa wale waliobatizwa kuwa Wakristo ikabidi wawataliki wake wa ziada kubaki na mmoja.
"Wakoloni wa Kiingereza wakazidi kuitokomeza zaidi mitala wakati walipowabana watu weusi kulipa kodi kwa kila mke waliyekuwa naye na uhaba wa ardhi ukazidisha tatizo kwa kutotosheleza mitaala," Ntshangase anasema.
Alipoulizwa iwapo ataruhusu mmoja wa wake zake kupata mume mwingine?
Musa alijibu: “Hapana, hakika nitakufa hilo likitokea.”
Thobile (28), ambaye pia amemueleza mumewe kama mume mwenye heshima na mwaminifu, husaidia kuendesha biashara mbalimbali za familia na huwa mgeni mwalikwa katika kipindi cha kila wiki redioni cha Gagasi FM, ambao huzungumzia kuhusu mapenzi, uhusiano na ndoa.
Thobile anasema kwamba nyendo za mumewe hazimsumbui. “Tumechagua maisha haya. Tumemchagua na tuko naye pekee. Hakuna mashindan o kati yetu.”
Je, kuna nafasi ya mke wa tano?
“Tunalitazama hilo na tutalizungumza katika kipindi hiki," Musa anasema.