28.3 C
Dar es Salaam
Monday, July 22, 2024

Contact us: [email protected]

MUHINGO AZIKWA

Na LEONARD MANG’OHA

-DAR ES SALAAM

MWILI wa mwanahabari mkongwe aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu (59), umeagwa na kuzikwa jijini Dar es Salaam.

Mazishi ya Muhingo aliyefariki Septemba 2, mwaka huu yalifanyika jana katika makaburi ya Kinondoni na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwamo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe.

Wengine ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk. Faustine Kamuzola, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, wakuu mbalimbali wa wilaya akiwamo wa Mkuu wa Wilaya ya Handeni aliyopata kuitumikia Muhingo, wawakilishi wa vyama vya siasa, maofisa wa serikali na waandishi wa habari.

Akizungumza wakati wa kuaga mwili wa marehemu Dk. Mwakyembe alisema Muhingo ni miongoni mwa vijana waliokuwa wamekomaa katika taaluma ya uandishi wa habari.

“Katika taaluma hii Muhingo ni mwalimu wa walimu ameondoka, nilimfahamu kwa muda mrefu wakati anakuja kijijini kwetu kumtembelea kaka yake.

“Nakumbuka Juni nami nikiwa nauguza pale Aga Khan nilikutana na mke wake akaniambia ndugu yako naye yuko wodini amelazwa nikapata nafasi ya kukaa naye akanieleza mambo mengi nami nikamtia moyo” alisema Dk. Mwakyembe.

Alisema serikali imeguswa na kifo cha mwandishi huyo aliyewahi kuwa Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd inayomilikia magazeti ya Mtanzania, Rai, Bingwa na Dimba.

Rafiki wa marehemu na Mhariri Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Absalom Kibanda, alisema kuwa kifo cha Muhingo ni sawa na kupoteza tanuru la fikira, mwalimu na kaka kwa waandishi wa habari na tasinia kwa ujumla.

“Kwa umuhimu wa Muhingo katika kipindi hiki naweza kusema tumepoteza mtu ambae huenda umuhimu wake haukufahamika mapema.

“Japo tulitofautiana katika hoja kadhaa za kimsingi lakini tulisaidiana kwa mambo mengi. Ndiye aliyenikutanisha na viongozi mbalimbali wa kisiasa, kwa kuwa alikuwa akipenda moja ya kitabu chenye kichwa ‘Mwalimu Nyerere hawezi kufa’ nami pia naamini Muhingo hawezi kufa.

“Nimeishi na Muhingo ndani na nje ya vyumba vya habari, na ninapozungumza hapa namwona Salva Rweyemamu wao ndiyo walionipokea na kunifundisha mambo mengi yaliyonijenga kitaaluma” alisema Kibanda.

Mbali na kufanya kazi pamoja na marehemu Kibanda alisema walikuwa marafiki na walishirikiana katika masuala mbalimbali ya kifamilia ikiwamo kusimamia masuala ya ndoa ya marehemu.

Akiongoza misa takatifu ya kuagwa kwa mwili wa marehemu iliyofanyika katika Kanisa la kiinjili kilutheri Tanzania, Usharika wa Mbezi Luis, Mchungaji Godlisten Nkya, aliwataka kutumia kifo cha Muhingo kujitafakari namna ambavyo wanaishi duniani.

“Ungelimwambia Muhingo leo hatokuwapo duniani katika umri huu nani angekuelewa lakini ukweli ndiyo huo” alisema Mchungaji Nkya.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Salum Mwalimu, alitumia nafasi hiyo kuwataka waandishi wa habari wanaoteuliwa kushika nafasi mbalimbali pamoja na viongozi wa serikali na taasisi mbalimbali kukumbuka walikotoka na kuthamini mchango wa taaluma ya habari.

“Tuko hapa viongozi wa vyama na kada mbalimbali kila mmoja akumbike alikotoka bila waandishi wa habari hakuna ambaye angemfahamu mwalimu” alisema Mwalimu.

“Mwenyekiti wetu Mbowe na Katibu Mkuu wa chama Vicent Mashiji wamepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha Muhingo. Alikuwa kaka, mwalimu hata kwetu ambao hatukufanya naye kazi alikiwa mtu muhimu kwetu kama chama cha siasa.

“Ametutoka wakati usio sahihi, mwandishi aina ya Muhingo alihitajika kuwapo ili kutuvusha kipindi hiki kigumu kwa tasnia ya habari” alisema.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kanali Mstaafu, Ngemela Lubinga, alisema chama chake kinatoa heshima ya pekee kwa marehemu Muhingo kwani alikuwa mtu muhimu aliyewasaidia.

Kanali Lubinga alitumia nafasi hiuo kuwaasa waandishi wa habari kuanzisha mfuko maalumu utakaowasaidia watoto wao pale wanapokuwa wamefikwa na mauti, kauli iliyoungwa mkono na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles