23.3 C
Dar es Salaam
Thursday, June 13, 2024

Contact us: [email protected]

MANJI, WENZAKE WAREJESHWA GEREZANI

NA KULWA MZEE

-DAR ES SALAAM

MFANYABIASHARA Yussuf Manji na wenzake watatu waliokuwa mikononi mwa polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, wamerejeshwa Gereza la Ukonga.

Washtakiwa hao walirejeshwa jana asubuhi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kuombwa na polisi kuhojiwa ili kukamilisha upelelezi wa kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili.

Mahakama iliamuru washtakiwa hao kwenda kuhojiwa baada ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa kanda hiyo, kuwasilisha barua mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, akiomba kukabidhiwa washtakiwa hao kwa lengo la kukamilisha upelelezi.

Hatua ya washtakiwa hao kukabidhiwa kwa polisi, iliambatana na hoja za kisheria zilizowasilishwa na upande wa Jamhuri na utetezi.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi, alidai kwamba wiki iliyopita waliomba washtakiwa kuletwa mahakamani ili waweze kuchukuliwa na kuhojiwa kuhusu kesi namba 33 ya mwaka huu ya uhujumu uchumi.

Kishenyi aliomba wakabidhiwe kwa polisi kwa kuwa wapo mikononi mwa magereza ili kuweza kutimiza takwa hilo, kwa kutumia kifungu cha 59(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

Kwa upande wa mawakili wa utetezi, Seni Malimi, Hajra Mungula na Hudson Ndusyepo, waliomba ombi hilo likataliwe na upande wa Jamhuri uelekezwe kujielekeza katika sheria kwa kutowaweka washtakiwa mahabusu kabla ya kukamilisha upelelezi.

Wakili Ndusyepo alidai mahakama hiyo haina mamlaka yoyote ya kutoa amri zilizoombwa na upande wa Jamhuri kwa sababu kesi hiyo haijapewa kibali na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) cha kuipa mamlaka ya kuyasikiliza.

Wakili Hajra alidai washtakiwa wapo mahabusu na mahakama hiyo ina jukumu la kuangalia na kulinda haki zao.

“Tunapata mawazo sana kwa kuwa washtakiwa wamewekwa mahabusu na kwa mbwembwe kabisa kwa kuweka hati ilhali upelelezi haujakamilika.

“Tunaiomba mahakama ikemee hali ya upelelezi bado, washtakiwa wanachukuliwa na kuwekwa ndani. Ombi likataliwe na upande wa Jamhuri waelekezwe kujielekeza katika sheria kwa kutomweka mshtakiwa ndani kabla ya kukamilisha upelelezi,” alidai Hajra.

Akijibu, Kishenyi alidai ni sahihi mahakama ina jukumu la kuwalinda washtakiwa, lakini hilo haliwezi kutafsiriwa kwamba maombi kama hayo yasifanyike na aliomba yakubaliwe kwa sababu siku zote mahakama inasisitiza juu ya kukamilisha upelelezi na hiyo ni sehemu ya kufanya hivyo.

Hakimu Shaidi alisisitiza kwamba hali ya washtakiwa iendelee kuwa kama walivyo kabla ya kuchukuliwa na polisi, wawe na afya njema na amani na wana haki ya kuwakilishwa na mawakili wao.

“Siku zote mahakama inapiga kelele upelelezi kukamilishwa kwenye kesi zikiwemo za uhujumu uchumi na hata kwenye kesi hii, hivyo kukataa ombi hilo ni kwenda kinyume na hilo.

“Nikisema nikatae, tutakuwa tunapingana na nia ya mahakama na hii si kesi ya kwanza washtakiwa kukabidhiwa kwa polisi ili kuhojiwa,” alisema Hakimu Shaidi.

Pamoja na mabishano hayo yote, Hakimu Shaidi alikubali ombi hilo la kuwakabidhi, Manji na wenzake kwa Koplo Dotto saa sita mchana na kutakiwa kurejeshwa jana ndani ya muda wa kazi.

Mbali na Manji, washtakiwa wengine kwenye kesi hiyo ambao walikabidhiwa kwa polisi ni Deogratius Kisinda, Abdallah Sangey na Thobias Fwere.

 

Katika kesi hiyo, Manji na wenzake wanakabiliwa na mashtaka saba chini ya sheria ya uhujumu uchumi na usalama wa taifa kwa kukutwa na vitambaa vinavyotumika kutengeneza sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 200 na mihuri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles