27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Kishoa ahoji wabunge kuzuiwa kufanya mikutano

Na MAREGESI PAUL

-DODOMA

MBUNGE wa Viti Maalumu, Jesca Kishoa (Chadema), amehoji ni kwanini wabunge wa viti maalum wanazuiwa kufanya mikutano ya hadhara katika mikoa wanayotoka.

Amesema kitendo hicho hakiwatendei haki wabunge hao na pia kinaonesha ubaguzi wa wazi kwa wabunge wanawake.

Kishoa aliyasema hayo bungeni jana baada ya kuomba mwongozo wa Spika akionesha kutoridhishwa na kauli iliyotolewa juzi na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, katika moja ya vikao walivyovifanya mjini hapa.

“Machi mwaka huu, wakati wa kipindi cha maswali na majibu, Mbunge wa Viti Maalum, Sophia Mwakagenda aliuliza swali lililohusu mikutano ya hadhara kwa wabunge wa viti maalum na kujibiwa majimbo ya wabunge hao ni mikoa wanayotoka.

“Lakini, jana katika kikao, Waziri wa Mambo ya Ndani alisema wanaoruhusiwa kuhutubia katika mikutano ya hadhara ni wabunge wa majimbo ila wabunge wa viti maalum wanaruhusiwa kuhutubia katika mikutano ya ndani ya vyama vyao.

“Kwa hiyo, mheshimiwa Spika, nasema huu ni ubaguzi wa wazi wazi na udhalilishaji wa wanawake kwa sababu sisi ni wabunge kama wabunge wa majimbo na ndiyo maana mishahara tunalipwa sawa.

“Hivyo basi, kama haturuhusiwi kufanya mikutano katika mikoa yetu, basi mtuambie tuondoe bendera katika magari yetu tunapokuwa nje ya mikoa yetu,”alisema Kishoa.

Akijibu mwongozo huo, Spika Ndugai alisema kanuni za Bunge hazitambui wabunge wa viti maalum wa mikoa, bali zinatambua uwepo wa wabunge wa viti maalum.

Kutokana na hali hiyo, alisema wanaoruhusiwa kuhutubia mikutano ya hadhara ni wabunge wa majimbo katika majimbo yao kwa kuwa ndiyo waliochaguliwa na wananchi.

“Kanuni za Bunge hakuna mahali zinakosema kuna wabunge wa viti maalum wa mikoa nawaomba acheni kukariri mambo haya.

“Mbunge wa viti maalum jimbo lako ni mkutano wa ndani wa chama chako wala si kwenye mkutano wa hadhara wa jimbo la mbunge mwingine.

“Wenye haki ya kuhutubia mikutano ya hadhara katika majimbo ni wabunge wa majimbo kwa sababu wao ndio waliochaguliwa na wananchi.

“Kwa hiyo, nadhani kuna haja sasa siku moja ifanyike semina kwa wabunge wa viti maalum pale Msekwa ambapo mimi na Waziri Mkuu tutahudhuria ili tuweke sawa mambo haya,” alisema Spika Ndugai.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles