JOHANES RESPICHIUS Na FRANCIS GODWIN-DAR ES SALAAM
MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amesema Benki ya Wanawake nchini imeipatia sifa kubwa Tanzania na hivyo kuifanya nchi kupata zawadi katika mkutano wa Umoja wa Afrika (AU).
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati akifungua Tamasha la 14 la Kijinsia lililoandaliwa na Mtandao wa Kijinsia Tanzania (TGNP), Samia alisema Tanzania imepata sifa kubwa barani Afrika hasa katika nyanja ya uwezeshaji wanawake kiuchumi.
“Hivi karibuni nilihudhuria katika mkutano wa Umoja wa Afrika, Tanzania tulipewa zawadi kutokana na kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia Benki ya Wanawake.
“Kama mnavyojua Serikali imeendelea kufanya jitihada mbalimba za kuwainua wanawake kwa kuanzisha mifuko ya uwezeshaji, saccos na vikoba,” alisema.
Alisema licha ya benki hiyo kuonekana kulegalega, serikali imejipanga kuifufua ili iweze kusimama na kufanya kazi kulingana na malengo na kwamba haitawasaidia wanawake tu bali hata wanaume watafaidika nayo.
Aidha Samia amelitaka Jeshi la Polisi nchini kuchukua hatua ya kupambana na unyanyasaji wa kijinsia katika jamii.
Alisema kuwa ukatili wa kijinsia unaofanywa na baadhi ya wanaume umezidi kuongezeka.
Alimtaka Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Lazaro Mambosasa kukomesha vitendo vya ukatili wa kijinsia ambavyo vimekithiri jijini humo.
“Serikali haitapenda kuona vitendo hivi vinaendelea katika jamii na kama wewe utashindwa kuchukua hatua kwa kuwawajibisha wa chini yako, utawajibika wewe hivyo anza sasa kupambana na vitendo hivyo kwa kuagiza wa chini yako,”alisema.
Samia alisema pamoja na kuongezeka kwa matukio ya ukatili wa kijinsia katika jamii bado wanaume wameendelea kufanya vitendo hivyo vya kikatili kwa wake zao kwa kuwapiga na hata kuwachoma moto.
“Suala la mila na desturi kwenye jamii yetu linapewa kipaumbele zaidi na kazi ya mwanamume ni kuishi kwa upendo na mke wake na si kumpiga mara kwa mara.
“Mwanamke akipigwa mara moja ama kuonywa mara moja inatosha si kumpiga kila wakati ama kumfanyia vitendo vya kinyama …ila hata sisi wanawake tunapaswa kuheshimu waume zetu.
“Mimi pamoja na nafasi yangu ya umakamu wa Rais, bado mume wangu nampigia magoti na kumnyenyekea tuishi kwa kuheshimiana.
“Sote ni mashahidi kuwa Tanzania ni mwanachama wa UN na AU imeridhia mikataba ,itifaki na makubaliano mbalimbali ya kimataifa na kikanda kuhusu suala la kijinsia na uwezeshwaji wa wanawake ambayo ni utekelezaji wa mpango kazi wa ulingo wa Beijing na mingine,”alisema.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP-Mtandao, Lilian Liundi alisema tamasha la mwaka huu linaongozwa na mada kuu ambayo ni mageuzi ya mfumo kandamizi kwa usawa wa jinsia na maendeleo endelevu.