Na SARAH MOSES-DODOMA
MTOTO Akisa Wilsoni (7), mkazi wa Mtaa wa Ilazo Kata ya Ipagala jijini Dodoma, amenusurika kifo baada ya kung’atwa na mbwa wanne sehemu mbalimbali za mwili wake na kumsababishia majeraha.
Akizungumza jana na MTANZANIA, Baba wa mtoto huyo, Wilsoni Moyo alisema tukio hilo lilitokea Mei 20, mwaka huu huku akieleza kuwa si la kwanza kutokea katika mtaa wao.
Alisema tukio hilo lilitokea wakati mtoto huyo akiwa na wenzake wakitoka nyumbani kuelekea kanisani, ndipo wakakutana na mbwa hao ambao walianza kumshambulia na kumvutia kichakani.
“Wakati tukio hilo likiendelea mara akatokea mama mmoja aliyekuwa akipita njia hiyo, akaanza kupiga kelele za kuomba msaada na ndiye aliyesaidia kumnusuru mwanangu kwa sababu wale mbwa walikuwa wameanza kumvutia kichakani,” alisema Moyo.
Mama mzazi wa mtoto huyo, Prudensiana Masima ambaye alizungumza na gazeti hili akiwa wodini alikolazwa mtoto wake, katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma alisema hali ya mtoto wake inaendelea vizuri tofauti na ilivyokuwa awali.
“Kwa sasa mtoto anaendelea vizuri tofauti na ilivyokuwa awali ingawa bado ana majeraha makubwa mwili. Nawashukuru madaktari wanamtibia mwanangu vizuri mpaka anaweza kula na kuongea.
“Namuomba sana mwenyekiti awaondoe mbwa wote ambao hawafugwi kwa sababu wamekuwa tishio mtaani kwetu na hasa kwa watoto wanaoenda shule,” alisema.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Ilazo, Mussa Thabiti alisema taarifa za kuwepo kwa mbwa hao anazo na tayari ameishachukua hatua kwa kuwaita maofisa wa halmashauri ambapo waliwaua kwa kuwapiga risasi.
“Hawa ni mbwa koko wanaozurura tu mtaani, hawana mahali pa kukaa ndiyo maana wanapigwa risasi, kama wangekuwa wanafugwa na watu basi tungeishawakamata na kuwachukulia hatua,” alisema