26 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

MSIGWA AMKUMBUKA MSAMBATAVANGU

Na RAYMOND MINJA- IRINGA


MBUNGE wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, amemkumbuka aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM  Mkoa wa Iringa,  Jesca Msambatavangu, Jah People na Abeid Kiponza, akisema wakati wa uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), hawakuonyesha uadui kwa upinzani kama ilivyo sasa.

Mchungaji Msigwa aliyasema hayo kwa wanahabari jana alipokuwa akizungumzia mustakabali wa siasa za Iringa na kamatakamata aliyodai kufanywa na Jeshi la Polisi kwa Chadema kwa lengo la kuibeba CCM.

Alisema ametoa malalamiko kwa Mkuu wa Polisi Nchini (IGP), Simon Sirro na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz, kuhusu jeshi hilo linavyofanya kazi mkoani humo.

“Tumefanya siasa na Jah People, Kiponza na Jesca, ilikuwa ni kawaida tukimaliza siasa tunapeana mikono na mambo mengine yanaendelea pasipo hila yoyote,” alisema.

Msigwa alisema hivi karibuni jeshi hilo liliwakamata wafuasi wa chama chake kwa maelekezo ya CCM na kuwafikisha mahakamani baada ya siku nane, wakiwahusisha na tukio la kuvunja nyumba ya Diwani wa Kata ya Mwangata aliyejiuzulu, Anjelus Mbogo na kuchoma nyumba aliyokuwa akiishi Katibu wa UVCCM Iringa Mjini, Alphonce Muyinga bila kufanya uchunguzi.

Katika kesi hizo, Mchungaji Msigwa alisema amehusishwa pia katika kesi ya kuchoma nyumba ya katibu huyo katika tukio lililotokea akiwa nje ya Mkoa wa Iringa.

“Waliponiita polisi niliwaambia sikatai wahalifu wanaweza kuwepo Chadema, lakini pia wanaweza kuwepo CCM, wasio na vyama na matukio kama hayo yanaweza kuwa ya kupangwa na wahusika kwa malengo ya kisiasa au ya kiuchumi, kwa hiyo kabla ya kamatakamata ni muhimu  wakafanya kazi yao kwa weledi na utulivu,” alisema.

Mchungaji Msigwa alikwenda mbali zaidi akisema anazo taarifa kwamba, matukio hayo yanatengenezwa na CCM kwa lengo la kuichafua Chadema baada ya mipango yao ya kuwashawishi na kuwanunua baadhi ya madiwani wa chama hicho kuanza kuonekana hayawaongezei umaarufu.

“Iringa siwezi kuondoka kwa mkono wa mtu, nitaondoka kwa mapenzi ya Mungu, mwanadamu hawezi kuniondoa, niliwekwa kwa mpango wa Mungu na nitaondoka kwa mpango wa Mungu,” alisema.

Msigwa alisema kasi ya wakazi wa Manispaa ya Iringa kuikataa CCM ilipamba moto wakati wa Uchaguzi wa Serikali za mitaa wa mwaka 2014 ilipopoteza mitaa 65 na ikaendelea kwa nguvu kubwa, katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 ilipopoteza halmashauri na Jimbo la Iringa kwa mara ya pili mfululizo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles