Na ESTHER MNYIKA – DAR ES SALAAM
KUJENGWA kwa viwanda vya kuzalisha dawa na vifaa tiba nchini kutasaidia kutatua changamoto ya kukosekana kwa dawa hospitalini na kuleta ufanisi wa upatikanaji kwa Watanzania.
Katika kuelekea Tanzania ya viwanda, Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ipo kwenye mchakato wa kuanzisha viwanda vya kuzalishia dawa na vifaa tiba nchini kupitia mpango wa ushirikiano na sekta binafsi katika ubia.
Kujengwa kwa viwanda vya kuzalisha dawa na vifaa tiba nchini kutapunguza gharama za kuagiza dawa nje ya nchi kama ilivyo kwa sasa.
Kutokana na hali hiyo ya kuendeleza viwanda, MSD ipo kwenye hatua za mwisho za kukamilisha upatikanaji wa kiwanja chenye ekari 100 katika eneo la Misugusugu, Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda hicho.
Akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu, anasema bohari hiyo imeanzisha mchakato wa kujenga viwanda hivyo nchini kupitia mpango wa ushirikishwaji wa sekta binafsi.
Anasema dawa na vifaa tiba vinavyotegemewa kuanza kuzalishwa katika awamu ya kwanza ni pamoja na IV fluids, Syrups, Cotton Wools na Surgical gloves.
Anasema kwa mda mrefu MSD katika Kanda ya Dar es Salaam, imekuwa inakabiliwa na ufinyu wa eneo la kuhifadhia dawa na vifaa tiba, hivyo kulazimu kukodi maghala ambayo yamekuwa yakiigharimu MSD takribani Sh bilioni 4 kwa mwaka.
Anasema kutokana na hali hiyo, Rais Dk. John Magufuli aliahidi kutoa eneo kwa ajili ya kuepuka gharama hizo na baada ya ahadi hiyo Machi mwaka jana, Waziri wa Ardhi na Mendeleo ya Makazi, William Lukuvi, aliikabidhi MSD hati ya kiwanja cha ukubwa wa ekari tano kilichopo eneo la Luguruni Wilaya ya Ubungo, kwa ajili ya ujenzi na upanuzi wa maghala na ofisi.
Anasema hata hivyo MSD itaendelea kukaribisha wawekezaji wanaotaka kuongeza wigo wa uzalishaji kulingana na uwezo wao wa kifedha na kiteknolojia.
“Sisi kama MSD tunatoa ardhi na soko kwa wawekezaji ila ni lazima utengeneze dawa na vifaa tiba vyenye viwango na ubora ili kupata soko kwa urahisi kwa wateja kutokana na bidhaa kuwa nzuri,” anasema Bwanakunu.
Anasema watu binafsi na wadau wanatakiwa kufungua viwanda vingi vya dawa ili kupunguza kuagiza dawa nje ya nchi.
Bwanakunu anasema MSD wameanza utaratibu wa kununua dawa na vifaa tiba moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji na kuhakikisha kuna upatikanaji endelevu na kupunguza gharama za ununuzi wa dawa hizo ambazo asilimia 80 zinatoka nje ya nchi.
Anasema utaratibu huo utasaidia kupunguza gharama za ununuzi wa dawa na vifaa kutoka kwa wafanyabiashara.
“ Hata hivyo, MSD hadi sasa imeshatoa mikataba 58 ya ununuzi wa dawa muhimu mbalimbali kutoka kwa wazalishaji wa ndani na nje ya nchi na wanatafuta wazalishaji 78 wa dawa na wazalishaji 76 ni wa vifaa tiba,” anasema.
Anasema kwa sasa wanahitaji kuhamasisha wawekezaji kwa sababu wana faida nyingi iwapo mitaji yao itakua na manufaa.
Anasema katika kuhakikisha inaongeza ufanisi katika shughuli za upokeaji , utunzaji na usambazaji wa dawa na vifaa tiba, MSD imeendelea kuboresha mfumo wa msimbo pau ‘barcode’.
Anasema mfumo huo ni wa kisasa utakaosaidia katika shughuli za ugavi wa dawa na vifaa tiba.
Anasema MSD wameanzisha mpango wa huduma maalumu kwa wateja wake wakubwa wenye lengo la kuwawezesha wateja hao kupata huduma kwa haraka zaidi pindi wanapokuwa wanahitaji dawa.
Bwanakunu alitaja baadhi ya wateja hao kuwa ni pamoja na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Taasisi ya Mifupa (MOI), Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Hospitali ya Bugando, Hospitali ya Mirembe, Hospitali ya Kanda ya Mbeya, KCMC, Hospitali ya Amana, Temeke, Mwananyamala, Mnazi Mmoja na nynginezo.
Aidha, anasema ndani ya mwaka jana MSD ilifanikiwa kufungua maduka saba ya dawa sehemu mbalimbali nchini.
Anasema lengo la kufungua maduka hayo ni kuziwesha hospitali ambazo ndio wateja wakubwa wa kununua dawa kwa ajili ya hospitali.
Anasema maduka ambayo hadi sasa yamefunguliwa ni pamoja na liliopo ndani ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Sekou Toure (Mwanza), Rufaa Mbeya na nyinginezo.
Bwanakunu anasema katika kipindi cha nyuma, kulikuwa na tatizo la ufinyu wa bajeti lakini kwa sasa hakuna tena changamoto hiyo.
“Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016\17 ilikuwa Sh bilioni 29, ambapo kila mwezi ninapewa Sh bilioni 2 kwa ajili ya kununua dawa na katika bajeti ya mwaka wa fedha ijayo ni Sh bilioni 251 na kila mwezi nitapewa Sh bilioni 21.8,” anasema.
Anasema wanasambaza dawa nchi nzima na wanatumia Sh bilioni 3 kwa mwaka na wana magari 100 kwa ajili ya kazi hiyo.
Anasema Serikali imetenga bajeti kubwa yenye kukidhi kasi ya uingizaji dawa nchini, hadi kufikia mwishoni mwa mwaka jana hali ya upatikanaji wa dawa nchini ilikuwa wa kuridhisha.
“Hadi kufikia mwishoni wa mwezi huu, aina 17 za dawa zitawasili na hali itatengemaa kwa asilimia 86, Februari mwaka huu aina tatu za dawa zitawasili hivyo kuboresha upatikanaji wa dawa kwa asilimia 88.