Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Vifo 2,648 vitokanavyo na uzazi vimeokolewa katika Mikoa 10 ya Dar es Salaam, Dodoma, Katavi, Iringa, Tabora, Mara, Kilimanjaro, Singida, Mbeya na Songwe baada ya Serikali kwa kushirikiana na wadau kutekeleza mradi wa uboreshaji huduma jumuishi za afya ya uzazi kwa wanawake (Wish2Action).
Mradi huo ulioanza Septemba 2018 hadi Desemba 2023 ulitekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali, Chama cha Uzazi na Malezi Bora Tanzania (Umati) na Marie Stopes.
Akizungumza Januari 26,2024 wakati wa kufunga mradi huo Mkurugenzi Mtendaji wa Umati, Suzana Mkanzabi, amesema mbali ya kuokoa vifo hivyo pia umeokoa mimba zisizotarajiwa 1,685,092.
“Shabaha kubwa ya mradi ilikuwa ni kuongeza matumizi ya kisasa ya njia za uzazi wa mpango na kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi. Tunatamani sana Serikali izungumze na wadau na kuwaeleza changamoto bado zipo hivyo, waendelee kufadhili ili tuendeleze juhudi tulizozianza,” amesema Mkanzabi.
Amesema kupitia mradi huo watu 3,871,615 wamefikiwa kwa kupatiwa elimu ambapo vijana ni 1,132,985 wakati vijana balehe ni 645,970 na watu wenye ulemavu ni 2,459.
Aidha amesema wametoa vifaa tiba kwa vituo 300 na kuwajengea uwezo watoa huduma za afya 286 na watoa huduma ngazi ya jamii 300.
Mkurugenzi wa Huduma za Afya Marie Stopes, Dk. Geofrey Sigalla, amesema kulikuwa na ushirikishwaji wa hali ya juu wa Serikali na kisekta hatua iliyowezesha kufikiwa kwa malengo ya mradi huo.
Mganga Mkuu wa Jiji la Mbeya, Dk. Elizabeth Nyema, amesema mradi huo umewasaidia kujenga uwezo wa watumishi na eneo la uchakataji takwimu na kwamba wataendelea kutumia mbinu zilizokuwa zikitumika katika mradi huo kuboresha huduma za uzazi.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara, Msalika Makungu, amesema wataendelea kusimamia uendelevu wa huduma hiyo ili kuhakikisha mazuri yaliyopatikana yanaendelezwa kupitia mipango na bajeti za halmashauri.
“Mafanikio yaliyopatikana tujitahidi kadiri inavyowezekana kuhakikisha tunayaendeleza kulingana na uwezo wetu wa kibajeti,” amesema Makungu.
Mratibu wa Huduma za Afya ya Mama na Mtoto Tamisemi, Dk. Yahaya Hussein, amesema mikoa ambayo imenufaika ilihitaji nguvu ya ziada kupandisha kiwango cha matumizi ya huduma za uzazi wa mpango.
“Tuliweka msisitizo eneo la utoaji wa huduma za uzazi wa mpango baada ya mama kujifungua, tulikuwa hatufanyi vizuri kama nchi.
“Mradi umetuachia alama nzuri ya vifaa tiba ambavyo vitasaidia kuendelea kutoa huduma kwa Watanzania,” amesema Dk. Hussein.