28.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 10, 2024

Contact us: [email protected]

Fuata taratibu hizi kutambua uhalali wa baba kwa mtoto

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) imeeleza taratibu za uchunguzi wa vinasaba ikiwemo kutambua uhalali wa watoto kwa wazazi ikisema anayehitaji kupatiwa huduma hiyo ni lazima awakilishwe kisheria.

Kifungu cha 25 (2) cha Sheria ya Vinasaba vya Binadamu ya mwaka 2009 kinataja taasisi zinazoruhusiwa kumuombea mteja kupatiwa huduma hiyo kuwa ni maofisa ustawi wa jamii, mawakili, mahakama, jeshi la polisi na nyingine.

Akizungumza Januari 29,2024 na Mtanzania Digital katika Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam Kaimu Meneja wa Maabara ya Sayansi Jinai Toksikolojia, Kagera Ng’weshemi, amesema taratibu hizo zimewekwa ili kuepusha migogoro katika jamii.

“Mtu anayetaka kupima vinasaba lazima apitie kwa mwanasheria anayetambulika ambaye ataandika barua kwa mkemia mkuu kuomba kutambua uhalali wa mtoto kwa baba.

“Suala lenyewe ni zito linahusu usalama katika jamii hivyo, inabidi lipitie mahala ambapo mtu atapata kwanza uelewa, ajue faida ya kupima au kutopima ili kuwa na uhakika kwamba hatua zote zinakwenda katika njia iliyo salama,” amesema Ng’weshemi.

Aidha amesema matokeo ya uchunguzi wa uhalali wa watoto kwa wazazi ni ya uhakika kwa sababu wanatumia mashine za kisasa na utaalamu wa hali ya juu.

“Tuna maabara yenye ithibati ambayo inatambulika kimataifa hivyo, matokeo utakayoyapata hata ukienda kwingineko duniani yatakuwa ni hayo hayo,” amesema.

Kwa mujibu wa mamlaka hiyo, gharama za uchunguzi ni Sh 100,000 kwa sampuli ya mtu mmoja hivyo kwa uchungizi wa baba, mama na mtoto ni Sh 300,000 na majibu hutolewa kuanzia siku ya kwanza hadi ya 21 baada ya kuchukuliwa kwa sampuli.

Kaimu meneja huyo amesema teknolojia ya vinasaba inahusika pia kufanya utambuzi wa makosa ya jinai kama vile matukio mbalimbali ya ubakaji, mauaji, kujeruhiwa na mengine ambapo uchunguzi hufanyika ili kutambua wahusika.

Amesema pia uchunguzi mwingine wa Vinasaba unahusika katika suala la upandikizaji figo na utambuzi wa jinsia tawala.

Katika maonesho hayo GCLA inaelimisha umma kuhusu shughuli mbalimbali inazofanya zikiwemo za kurugenzi ya huduma ya sayansi jinai, kurugenzi ya huduma za udhibiti na kurugenzi ya uchunguzi wa bidhaa na mazingira.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles