Na UPENDO MOSHA, MOSHI
SHIRIKA lisilo la kiserikali la TUSONGE, ambalo linajishughulisha na masuala ya uwezeshaji wa kiuchumi kwa makundi maalumu, yakiwamo ya wanawake na vijana, limezindua mradi maalumu wa kuwawezesha watu wenye ulemavu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo mjini Moshi jana, Mkurugenzi Mtendaji wa TUSONGE, Agnatha Rutazaa, alisema mradi huo umelenga kuwawezesha watu wenye ulemavu kiuchumi kwa kuwa kundi hilo lilikuwa limetengwa na taasisi za kifedha.
“Kundi hili limekuwa likisahaulika kwa asilimia kubwa na kutengwa na taasisi za kifedha pale zinapotokea fursa za kiuchumi, kwani watu hawa wamekuwa wakionekana kutokidhi vigezo vya kukopa kwa sababu ya hali zao, hivyo TUSONGE tumeliona hilo na kuja na mradi maalumu wa kuwakwamua kiuchumi,” alisema.
Alisema kwa sasa mradi huo utakuwa wa majaribio kwa muda wa miaka miwili na kwamba wanatarajia kuwafikia watu zaidi 360, ikiwemo wanawake wenye ulemavu 28, wanaume wenye ulemavu 10, wanawake na wasichana wasio na ulemavu 322.
“Mradi huu umefadhiliwa na mashirika mawili ya Serikali ya Uingereza, ambayo ni African Initiatives na Big Lottery Fund, lengo ni kuwaunganisha watu wenye ulemavu ili na wao wajione kama sehemu ya jamii na wajione wana mchango katika maendeleo ya jamii zao na taifa kwa ujumla,” alisema.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Shirika la African Initiatives, Valerie Msoka, alisema awali walikuwa wakifadhili miradi mingi kwa makundi ya watu mbalimbali, isipokuwa kundi la watu wenye mahitaji maalumu.
“Mradi huu umelenga watu wenye ulemavu na sisi tupo tayari kuwawezesha kupitia mikopo ili waweze kuendesha miradi yao mbalimbali,” alifafanua Msoka.
Kwa upande wake, Ofisa Mradi huo, Helena Mushi, alisema mradi huo utafanyika katika kata ya Njiapanda, Wilaya ya Moshi Vijijini.
Mmoja wa wanufaika wa mradi huo, Priscus Silayo, alisema kuwa, mpango huo utawakomboa kiuchumi na kuondokana na dhana ya kukaa barabarani na kuombaomba.