25 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

MOI yaitaka jamii kujitokeza kuchangia damu

Na AVELINE KITOMARY

TAASISI ya Mifupa Muhimbili (MOI) imewahimiza watu mbalimbali, kampuni na taasisi kujitokeza kuchangia damu ili kuokoa maisha ya wagonjwa wa dharura wanaofikishwa katika taasisi hiyo.

Akizungumza jana na MTANZANIA Jumapili, Ofisa Habari wa taasisi hiyo, Patrick Mvungi, alisema tangu kuingia kwa ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (Covid-19), idadi ya watu wanaochangia damu imepungua hali inayosababisha wagonjwa kukosa damu.

Alisema asilimia 90 ya wagonjwa waliopo katika taasisi hiyo hufanyiwa upasuaji, hivyo uhitaji wa damu ni mkubwa kwa sasa.

 “Utaratibu ni kwamba kama ndugu yako anaumwa unakuja kutoa damu ili aweze kufanyiwa upasuaji na mgonjwa kuongezewa damu, huu bado upo na hatujaufuta.

“Hapa tunaomba kupata damu kwa ajili ya wale wagonjwa wa dharura, mfano mtu kapata ajali, hapo mnampokea utakuta ameishiwa damu na anahitajika kuongezewa, lakini kwa wakati huo ndugu zake bado hawajui hata kama yuko hospitali, hawa ndio wanaohitaji msaada zaidi,” alisema Mvungi.

Alisema wameweka utaratibu maalumu ambao utasaidia wachangiaji kuepuka misongamano na kwamba taratibu zote za kujikinga zitafuatwa.

“Watu wajitokeze hata kama ni vikundi, tutaweka utaratibu maalumu ambao hautasababisha msongamano kwani watakuja kidogo kidogo, hivyo wasiwe na wasiwasi,” alisema Mvungi.

Alisema kuwa damu ni kitu pekee ambacho hakiwezi kununuliwa, hivyo amewataka wananchi walichukulie uzito suala hilo.

Aliwataka Watanzania kuwa na moyo wa upendo kwa kuokoa maisha ya wenzao kwa kuchangia damu, hasa majeruhi wa ajali ambao hufikishwa kwa dharura katika taasisi hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles