WINFRIDA MTOI, DAR ES SALAAM
ALIYEKUWA Kocha Msaidizi wa Yanga, Charles Mkwasa amepata ajira ya kuinoa timu ya Ruvu Shooting inayomikikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa(JKT).
Hiyo siyo mara ya kwanza kwa kocha huyo kuinoa Shooting, kwani aliwahi kufanya kazi katika kikosi hicho miaka ya nyuma.
Kabla ya kurejea Shooting, Mkwasa alikuwa akifanya kazi na Yanga akiwa kocha msaidizi, ambapo mkataba wake ulifikia tamati Agosti mwaka huu.
Akizungumza MTANZANIA jana, Ofisa Habari wa Ruvu Shooting, Masau Bwire, alithibitisha Mkwasa kupewa jukumu la kuifundisha timu yao, akifichua kuwa ataanza kazi rasmi kesho kutwa.
“Ni kweli Mkwasa ni kocha mpya wa Ruvu Shooting, anachukua nafasi ya Salum Mayanga aliyeondoka, ataanza kazi rasmi Jumatatu kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya,” alisema.
Alisema wana imani na Mkwasa kutokana na uzoefu wake katika Ligi Kuu Tanzania Bara.