23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Ukaribu wa Diamond, Zuchu kuna usalama?

Christopher Msekena

MWAKA 1988, akiwa na miaka 18, mwanamuziki nyota nchini Marekani, Mariah Carey, alikutana na bosi wa lebo ya Sony Music, Tommy Mottola ndani ya mgahawa aliokuwa anafanya kazi kama muhudumu jijini New York.

Wakati huo, Mariah Carey alikuwa akiishi maisha ya chini kwenye kitongoji cha Long Island huku kiu yake kubwa ikiwa ni kuwa mwimbaji maarufu duniani, hivyo kukutana na Mottola ilikuwa ni zari la mtende.

Mottola alifanikisha mchakato wa Mariah Carey kusaini dili na lebo ya Sony Music ambapo mwaka 90 akafyatua albamu yake ya kwanza iliyobadilisha maisha yake na kumpeleka levo nyingine kabisa kwenye tasnia ya muziki.

Taratibu mzee baba, Mottola akaanza kutupa kete yake kwa Mariah Carey, wakaanza kuonekana pamoja kwenye shughuli mbalimbali wakiwa kwenye ukaribu uliopitiliza. Paparazi wakanusa harufu ya penzi hilo zito baina ya wawili hao.

Tetesi za Mariah Carey kutoka kimapenzi na bosi wake, Mottola ziliposhika kasi na wakaamua kufanya kweli kwa kufunga ndoa mwaka 93 baada ya Mottola kuachana na mkewe wa kwanza, Thalia.

Sio Mottola pekee ndio bosi aliyewahi kutoka kimapenzi na msanii wake wa kike, wapo kibao akiwamo Tim Weatherspoon ambaye alimuoa msanii wake, Kelly Rowland na kiroho safi mpaka leo maisha yanaendelea wakiwa na miaka sita kwenye ndoa yao yenye furaha.

Unaweza kushangaa kwanini nimeanza na simulizi za mapenzi za wasanii wakubwa duniani na kuacha ishu kubwa ambayo ni gumzo mtaani ikimhusisha bosi wa WCB, Diamond Platnumz na msanii wake mpya, Zuchu.

Nilitaka nikuonyeshe kwamba si jambo la ajabu msanii wa kike kuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi au kuolewa na bosi anayesimamia kazi zake ilhali kuna maridhiano na mapenzi ya dhati baina yao.

Kwa muda mrefu sasa mitandao ya kijamii imekuwa ikipambwa na picha za matukio tofauti ambayo Diamond Platnumz ameongozana na Zuchu. Ukaribu wao ndio umechochea gumzo na wadadisi wa mambo wameanza kuunganisha ‘doti’ ili kupata picha kamili kama ni kweli wawili hao ni wapenzi au laa.

Tangu WCB ilipomtangaza Zuchu kama msanii wao mpya, Diamond amekuwa mstari wa mbele katika kumnadi mrembo huyo popote pale anapopata nafasi, iwe kwenye mitandao ya kijamii au kwenye mikutano ya dili anayofanya na kampuni tofauti.

Wengine wameenda mbali kwa kuhoji kwanini Diamond amekuwa karibu zaidi ya Zuchu tofauti na wasanii wake wengine. Kipindi anatambulishwa Harmonize, Rayvanny, Mbosso, Queen Darleen na Lavalava, Mondi hakuwahi kuambatana nao kwa kiasi kikubwa kama anavyofanya kwa Zuchu.

Mfano ni Julai 18, mwaka huu Diamond alitangaza kuwa yupo singo na mashabiki wakae tayari kumwona mrembo wake mpya atakayepita naye kwenye ‘red carpet’ pale Mlimani City kwenye uzinduzi wa albamu fupi (EP), I Am Zuchu.

Wengine walitarajia Diamond atapita kwenye zuria jekundu na warembo ambao tunafahamu aliwahi kuwa nao kwenye mahusiano kama vile Zari The Boss Lady, Wema Sepetu, Hamissa Mobetto na wengineo lakini jamaa akawashangaza maahabiki kwa kuingia ukumbini na Zuchu.

Na kama unavyojua heshima ya zuria jekundu kwenye matukio makubwa yenye hadhi kama ile huwa zinapita kapo za mastaa. Hilo nalo likaongeza hisia kwa mashabiki kwamba kuna kitu zaidi ya kazi baina ya Diamond na Zuchu.

Hata kwenye harusi ya dada wa Diamond, Esma Platnumz, wawili hao walikuwa karibu zaidi tofauti kabisa na alivyowahi kuwa karibu na wasanii wengine wa lebo hiyo pindi wanatambulishwa WCB.

Wiki hii pia kwenye tukio uzinduzi wa muhuri wa usalama kwa wasafiri uliotolewa na Baraza la Wasafiri na Watalii Duniani (WTTC), Diamond kama kawaida yake aliambatana na Zuchu.

Jambo lililovutia zaidi ni pale ambapo Diamond alionekana akimfungulia mlango wa gari Zuchu. Wajumbe wanahoji toka lini Diamond akamfungulia msanii wake mlango wa gari maana hiyo ni kazi ya mabaunsa wake ambao pia kwa sasa wanamlinda na Zuchu.

Ndio maana mashabiki wameendelea kukoleza fununu za wawili hao kuwa kwenye dimbwi zito la mapenzi hasa kipindi hiki ambacho Diamond ametangaza kufunga ndoa hivi karibuni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles