NA CHRISTOPHER MSEKENA
SUALA la wasanii kuingia mikataba mibovu inayowanyonya na kuwanyima uhuru, imekuwa ikipigiwa kelele mara kwa mara na wadau katika sekta ya sanaa.
Jana tukio linalohusiana na mikataba mibovu ya kazi imemwibua mcheza sinema, Wastara Juma, baada ya kuingia mtakaba wa kuwa balozi wa bidhaa za kampuni ya simu ya KZG.
Wastara amedai kukimbiwa na kudhulumiwa na kampuni hiyo kutoka China kiasi cha shilingi milioni 80, baada ya kuifanyia kazi ya kutangaza simu hizo.
Akiandika waraka mrefu aliolenga umfikie Rais Dk. John Magufuli, Makamu wa Rais, Samia Suluhu, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na Watanzania wote juu ya kilio chake hicho, Wastara aliweka wazi hitaji lake la kuomba fedha kwa ajili ya kwenda nchini India kwenye matibabu ya mguu na mgongo vinavyomsababishia maumivu makali yanayomfanya apoteze fahamu mara kwa mara kwa kuwa amechelewa kwenda hospitali.
Kwa ufupi hana fedha ya kumwezesha kupata matibabu, hivyo matumaini yake yapo kwa viongozi hao aliowataja na wewe msomaji, naamini katika hilo atafanikiwa kwa kiwango cha juu.
Katika mkasa huo wa Wastara, kuna jambo ambalo ni muhimu kwa wasanii wengine kujifunza ili haya yaliyotokea kwa mwigizaji huyo yasitokee tena. Mikataba ya kibalozi kama hiyo iwe neema na si mwiba wa kuwachoma wasanii.
Ukirejea katika maelezo ya Wastara, ameweka wazi kuifanya kazi hiyo kama alivyotakiwa, lakini hakupata fedha zake ambapo mwaka jana Januari, Wachina hao walimkimbia.
Bila shaka hapo utaona ni namna gani wasanii wanapaswa kuwa makini na aina ya mikataba wanayoingia kwani Wastara licha ya kutolipwa fedha zake ameendelea kuwa balozi wa kampuni hiyo huku akishindwa kufanya kazi na kampuni nyingine kutokana na mkataba wa KZG kumbana.
Ni vyema wasanii wetu wakawatumia wanasheria katika masuala yanayohusisha mikataba ili kuepusha wasije wakatia saini kwenye mikataba inayowaumiza au kufanya kazi bila malipo au kukimbiwa kama alivyofanyiwa Wastara.
Nimalize kwa kuwaomba wadau wa sheria na viongozi wa sekta ya sanaa ukiwa ni pamoja na wewe msomaji, kufanya chochote kitu ili kumwezesha mwigizaji huyo apate matibabu na apate haki yake anayoidai kutoka kwenye kampuni hiyo ya simu.