30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

DK. SHEIN- ZANZIBAR ITAJITOSHELEZA KWA DAWA ZOTE IFIKAPO 2019

Na Mwandishi Wetu

RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema kuanzia mwezi Julai mwaka 2019, Zanzibar haitakuwa tena na tatizo la uhaba wa dawa kwa magonjwa yote yanayowakabili wananchi wake.

Alisema hilo linawezekana, kutokana na uchumi wa Zanzibar kuimarika hatua kwa hatua, hivyo wananchi wa Zanzibar wataondoka na shida waliyonayo hivi sasa ya uhaba wa dawa uliopo kwenye vituo vya afya pamoja na hospitali kadhaa.

Dk. Shein alieleza hayo jana baada ya kukifungua kituo kipya cha afya cha Michenzani Wilaya ya Mkoani, ikiwa ni shamra shamra za miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Alisema Serikali inapotoa ahadi zake kwa wananchi huzitekeleza kwa wakati, hivyo nalo tatizo la kuondoa uhaba wa dawa kwa mujibu wa magonjwa yaliyopo Zanzibar, linatarajiwa kuondoka kuanzia Julai mwaka 2019.

Dk. Shein alieleza kuwa zipo ahadi kadhaa amezitoa kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuipandisha hadhi Hospitali ya Abdalla Mzee na kuwa ya Mkoa sambamba na kuingiza vifaa vya kisasa jambo mbalo limeshakamilika.

Pia aliahidi kutekeleza ahadi yake ya kufuta michango ya elimu ngazi za shule za msingi na sekondari. Alieleza uchumi wa Zanzibar umekuwa ukikua siku hadi siku, licha ya ongezeko la idadi ya watu na mahitaji, kutoka watu 300,000 mwaka 1964 hadi sasa kufikia milioni 1.5.

“Kutokana na kuimarika kwa uchumi, leo natoa ahadi kwenu nyinyi wananchi, kuwa kuanzia mwezi wa saba mwaka 2019, dawa zote zitapatikana katika vituo vyote vya afya na hospitali za Serikali,” alisema.

Kuhusu matibabu, alisema Serikali inadhamiria kuleta kifaa cha kisasa cha kuchunguzia maradhi yote EMRI, kwenye Hospitali ya Mkoa ya Abdalla Mzee mkoani.

Kituo cha Afya cha Michenzani Wilaya ya Mkoani Pemba, ambacho awali kiliwekewa jiwe la msingi na rais huyo wa Zanzibar mnamo mwaka 2012, ambapo kilianza kwa nguvu za wananchi, ambapo pia wameshajengewa nyumba ya daktari kwa msaada wa Milele Foundation.

Mapema Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar, Halima Salum Maulid, alimpongeza Rais wa Zanzibar kwa hatua yake ya kuwaongezea fedha kwenye bajeti yao kuu, kutoka shilingi bilioni 7 hadi shilingi bilioni 10 kwa ajili ya ununuzi wa dawa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles