ELIZABETH KILINDI-NJOMBE
MKUU wa Wilaya ya Wanging’ombe, Mkoa wa Njombe, Ally Kassinge, ameshangazwa na kasi ya wanafunzi kupewa mimba wilayani hapa.
Amesema kwamba, kuanzia Januari mwaka huu hadi Mei mwaka huu, wanafunzi sita wamekatishwa masomo kwa sababu ya kupata mimba wakiwa shuleni.
Kassinge aliyasema hayo juzi katika kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe.
Alisema licha ya mikakati waliojiwekea kama wilaya kwa ajili ya kukabiliana na mimba za utotoni, bado changamoto hiyo inaendelea kujitokeza mara kwa mara, jambo ambalo alisema wanatakiwa kulifanyia kazi zaidi.
“Kama wilaya tulishajiwekea mikakati ya kukomesha mimba shuleni, lakini kwa masikitiko makubwa, nasema mwaka huu pekee kwa maana ya kuanzia Januari hadi Mei, wanafunzi sita wameacha masomo kutokana na kubeba mimba.
“Pia, zipo taarifa za mimba ambazo watendaji na wakuu wa shule au walimu wakuu hawaziwasilishi lakini mimi ninazipata taarifa hizo kupitia vyombo vyingine.
“Sasa hii si sawa, lazima taarifa hizi ziwasilishwe na tupate taarifa za hatua zilizochukuliwa dhidi ya waliowapa mimba wanafunzi hao,” alisema Kassinge.
Kutokana na hali hiyo, mkuu huyo wa wilaya aliagiza kata zote ambazo zina shule za sekondari na msingi, wafanye mapitio upya ili kujua ni wanafunzi wangapi wameacha masomo kwa sababu za ujauzito.
“Waliosababisha mimba hizo ni akina nani na wamechukuliwa hatua gani. Lakini, nitumie fursa hii kwa zile mimba sita nilizozipokea ofisini kwangu, natoa maagizo kwa mkuu wa polisi wilaya, afuatilie ili kujua hatua zilizochukuliwa dhidi ya wahusika. Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe, Antony Mawata (CCM), alisema wakati umefika kwa madiwani kusimamia mikakati waliyojiwekea kama halmashauri ya kukabiliana na mimba shuleni