Aveline Kitomary -Dar es salaam
DAKTARI bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Sulende Kubhoja, amesema kuwa mikusanyiko huweza kusababisha magonjwa ya moyo kwa watoto.
Dk. Kubhoja pia alisema kuwa endapo mtoto atazaliwa katika kituo cha afya, ataweza kuepuka kupata magonjwa ya moyo kutokana na kupata uangalizi na vipimo.
Akizungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalum, Dk. Kubhoja alisema ni vyema sasa wazazi wakazingatia maelekezo yanayotolewa na wahudumu wa afya ili kuepuka matatizo ya moyo kwa watoto.
“JKCI tunapokea wagonjwa nchi nzima, hata nje ya nchi, kwa wastani wa siku tunaona wagonjwa 30 kwa upande wa watoto. Kila siku tunafanya operasheni kwa watoto wawili kwa sababu zinachukua muda na gharama nyingi na katika wagonjwa 30 wanaokuja wengi wana hitilafu ya moyo ya kuzaliwa nayo na wanaobaki ni kutokana na magonjwa ya kuambukizwa.
“Kinga ni bora kuliko tiba, kuna vitu ambavyo tafiti zilishafanyika, kwamba kinga kwa kutumia chanjo inasaidia, hivyo tunahimiza watu kuchangamkia chanjo, kingine ni kuwakinga watoto na maambukizi, wanaweza kupata chanjo, lakini ni vizuri kuwazuia watoto wasiambukizwe,” alifafanua Dk. Kubhoja.
Alisema kwa sasa kumekuwa na wimbi kubwa la watoto kupelekwa shule za awali wakiwa kwenye umri mdogo, huku kukiwa na msongamano katika shule zao, hali ambayo ni hatari kwa afya ya moyo.
“Utakuta mtoto ana miaka miwili au mitatu bado hajajua kujitegemea, kujituza, kujisafisha na kule darasani wanakusanywa kwa pamoja, utakuta hapo mwingine anakohoa, mwingine kupiga chafya, wanaambukizana magonjwa ya njia ya hewa.
“Kwahiyo ni vizuri mtoto akianza shule kinga yake ya mwili iwe imara hivyo mikusanyiko haifai kwa watoto, tuwaepushe watoto na mikusanyiko mingi isiyokuwa na sababu na ndo maana haturuhusu watoto kutembelea wagonjwa hospitali kwa sababu wanaweza kuambukizwa magonjwa mengine,” alisisitiza Dk. Kubhoja.