Na Victoria Godfrey, Dar es Salaam
Serikali na wadau wa Michezo wameombwa kujitokeza kuisaidia timu ya Taifa ya Mieleka inayojiandaa na mashindano mbalimbali ya kimataifa.
Timu hiyo inaendelea na mazoezi Msasani Beach jijini Dar es Salaam ikijiandaa na mashindano ya kufuzu kushiriki Michezo ya Olimpiki itakayofanyika April 2 hadi 4, mwaka huu, na ya Ubingwa wa Afrika yatakayofanyika Aprili 6 hadi 11, mwaka huu, nchini Morocco.
Akizungumza na www.mtanzania.co.tz , Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mileleka ya Ridhaa Tanzania (TAWF), Abraham Nkabuka, ametaja mahitaji yao ni kupata fedha za kujikimu, usajili wa ushiriki, nauli ya kwenda na kurudi na vifaa vya mazoezi.
“Maandalizi yanaendelea vizuri, hivyo tunahitaji uwezeshwaji tunaomba wadau wajitokeze kwani milango ipo wazi kutusaidia gharama za usajili mtandaoni kwenye kufuzu Olimpiki mwisho Machi 2, mwaka huu na yale ya Afrika mwisho Aprili 6 mwaka huu,” amesema Nkabuka.
Ameongeza kuwa mahitaji mengine ni kupata leseni ambazo zitatumika kwenye mashindano hayo, hati ya kusafiria, vitu vidogo kama maji ya kunywa wakiwa mazoezini.
Naye Mchezaji, Latifa Kambi, ameahidi kuiwakilisha na kuipeperusha bendera ya Taifa kwenye mashindano hayo.
Ametoa rai kuwa wanawake kujitokeza kwa wingi kushiriki michezo kwa kuwa ni afya na ajira.
Kwa upande wake Nahodha wa timu ya Taifa, Geoffrey Michael, amewaasa wachezaji kuhakikisha wanafanya bidii kwenye mazoezi ili ibidisha kwenye kuweza kutimiza malengo yao.
Amesema wamejipanga vyema na kuwataka watanzania watarajie ushindi na kupata nafasi ya kusonga mbele na kushiriki Michezo ya Olimpiki mwaka huu