NA JENNIFER ULLEMBO, DAR ES SALAAM
KOCHA Mkuu wa timu ya Yanga, Hans van Der Pluijm, amesema atatumia michuano ya Kombe la Kagame kujifunza mbinu za kukisaidia kikosi chake katika michuano ya kimataifa ya Klabu Bingwa Afrika na siyo usajili.
Michuano ya Kagame inatarajiwa kufanyika hapa jijini Dar es Salaam Julai mwaka huu, kwa kushirikisha mabingwa wa klabu ambao ni wanachama wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
Akizungumza na MTANZANIA jana akiwa nchini Ghana kwa mapumziko, Pluijm alisema michuano hiyo ndiyo sababu iliyofanya akatishe likizo yake na kurudi nchini mapema ili kuanza kuiandaa timu yake.
“Nimejipanga kutumia michuano ya Kombe la Kagame kupata mbinu za michuano ya kimataifa ambayo tutashiriki mwakani na siyo kujiandaa na ligi msimu ujao,” alisema Pluijm.
Mholanzi huyo alisema hafikirii kufanya usajili kupitia michuano hiyo ya Kagame, kwani anatambua mchezaji mzuri hawezi kupatikana kiurahisi.
“Huwezi kupata mchezaji mzuri ambaye atakuletea mafaniko katika timu yako kupitia michuano kama Kagame, ingawa asilimia kubwa ya viongozi wa klabu Tanzania wamekuwa wakifanya hivyo,” alisema Pluijm.
Alisema anajiamini mapendekezo yake aliyowasilisha kwa uongozi yanatosha kuleta nguvu mpya katika timu hiyo, bila kutumia michuano ya Kagame kama usajili.
Pluijm anatarajiwa kurejea nchini Juni 7 mwaka huu, huku mipango yake ikiwa ni kuanza kukifua kikosi chake Juni 8, tayari kwa kushiriki michuano hiyo.