26.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Miaka 60 ya Uhuru| Serikali yaruhusu wanafunzi waliokatisha masomo kwa ujauzito kurejea shule

*Wanaofeli, kufanya udanganyifu darasa la saba kupata fursa nyingine

*Yakerwa na utitiri wa michango Dar

*Mitaala, elimu kwa wenye mahitaji maalum kuboreshwa

Na Ramadhan Hassan, Dodoma

WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeruhusu wanafunzi wa shule za msingi na sekondari waliokatisha masomo yao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kupata ujauzito kuendelea na masomo katika mfumo rasmi mara baada ya kujifungua mwaka unaofuata.

Uamuzi huo umetangazwa leo Jumatano Novemba 24,2021 jijini Dodoma na Waziri wa Wizara hiyo, Profesa. Joyce Ndalichako wakati akitaja mafanikio ambayo imeyapata Wizara hiyo katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara.

Waziri Ndalichako amesema Serikali itaendelea kuondoa vikwazo vya upatikanaji wa fursa ya elimu kwa wanafunzi kwa kutoa fursa kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari waliopewa ujauzito kurejea shuleni.

Prof. Ndalichako amesema Wanafunzi hao wataruhusiwa kuendelea na masomo yao katika mfumo rasmi wa seriaklli mara baada ya kujifungua.

“Serikali imeamua wanafunzi waliokatisha masomo yao kutokana na sababu mbalimbali watapewa fursa ya kurejea shuleni itajumlisha wasichana wanaopata ujauzito wakiwa katika shule za msingi na sekondari, wanafunzi hao wataruhusiwa kuendelea na masomo yao katika mfumo rasmi wa serikali mara baada ya kujifungua,”amesema Prof. Ndalichako.

WALIOFELI, WADANGANYIFU, WAPEWA FURSA

Pia amesema wanafunzi waliofeli, kufanya udanganyifu au kufukuzwa shule kwa utovu wa nidhamu watapewa fursa ya kurudia mitihani na watapewa fursa ya kujiunga na shule za sekondari.

“Utaratibu ulivyo sasa, mwanafunzi anapofutiwa mtihani wake wa darasa la saba au ambao atafeli mtihani wa darasa la saba au anapokuwa amepata tatizo lolote wakati wa mtihani wa darasa la saba atakuwa hana fursa nyingine, sasa tumeamua wanafunzi wanaofeli, kufanya udanganyifu au utovu wa nidhamu watapewa fursa ya kurudia mitihani na watapewa fursa ya kujiunga na shule za sekondari,”amesema Prof. Ndalichako.

ACHUKIZWA NA UTITIRI WA MICHANGO DAR ES SALAAM

Aidha,Prof. Ndalichako amezitaka shule ambazo zinawachangisha wanafunzi fedha za michango kuachana na utaratibu huo kwa sababu msimamo wa serikali ni kutoa elimu bila malipo.

“Na zaidi Dar es Salaam nimeambiwa kwamba michango imezidi Ilala, Kinondoni acheni kuchukua hela za wanafunzi wafundisheni wapate elimu na sio kuwabebesha utitiri wa michango jambo hili halikubaliki,”amesema.

MWELEKEO WA WIZARA NI KUTOA ELIMU BORA

Aidha, Waziri Ndalichako amesema Mwelekeo wa Sekta ya Elimu baada ya Miaka 60 ya Uhuru wa nchi ni kuendelea kutoa elimu bora itakayoipatia jamii maarifa na ujuzi unaokidhi mahitaji Kitaifa, Kikanda na Kimataifa.

UBORESHAJI WA MITAALA

Amesema serikali itahakikisha kwamba inaboresha mitaala ya elimu katika ngazi zote na kuweka msisitizo zaidi katika masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Sayansi, Ujasiliamali, Stadi za kazi na masuala mtambuka.

Waziri Ndalichako amesema fani za kimkakati kama vile uhandisi, kilimo, udaktari zitendelea kupewa kipaumbele.

Amesema serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya shule ili kuendelea kutoa fursa zaidi kwa watoto wa kike na wa kiume.

“Kazi hii inafanyika kwa kasi zaidi chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ambapo sambamba na ujenzi wa madarasa 15,000 unaoendelea nchini Serikali inatarajia kujenga shule 1,000 za sekondari za kutwa na  shule za sekondari 26 za wasichana katika kipindi cha miaka mitano ijayo,”amesema.

Waziri huyo amesema utekelezaji umeanza kwa shule 274 za kutwa na shule 10 za Wasichana ambapo serikali imetoa jumla ya Sh bilioni 1,405 mnamo tarehe Novemba, 2021.

ELIMU YA UFUNDI

Amesema elimu ya Ufundi na mafunzo ya ufundi stati itaendelea kuimarishwa ambapo kwa sasa Serikali inaendelea na ujenzi wa Vyuo vya ufundi stadi katika Wiaya 29 na Mikoa.

Amesema  lengo ni kutoa fursa zaidi kwa vijana kupata ujuzi na umahiri utakaowawezesha kujiajiri au kuajiriwa.

“Kwa msingi huo,mafunzo kwa vitendo yatapewa uzito stahiki sambamba na kuimarisha ushirikiano na viwanda ili kuhakikisha wanafunzi wanapata mafunzo yanayozingatia mahitaji halisi ya soko la ajira;,”amesema

ELIMU MAALUM  

Prof. Ndalichako amesema serikali itaendelea kuimarisha elimu maalum kwa kuhakikisha miundombinu inayojengwa ni rafiki kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Aidha, serikali itaendelea kununua vifaa visaidizi ili kuwawezesha wanafunzi wenye mahitaji maalum kujifunza kwa ufanisi zaidi.

Amesema serikali itaendelea kuondoa vikwazo katika upatikanaji wa fursa za elimu ambapo wanafunzi waliokatiza masomo yao kwa sababu mbalimbali watapewa fursa ya kurejea shuleni. Fursa hizo zitajumuisha wasichana ambao wanapata ujauzito wakiwa katika shule za msingi au sekondari.

Pia amesema Serikali itaendelea kutoa elimu bila malipo ili kuhakikisha kuwa watoto wote wakitanzania wanapata elimu bila vikwazo.

Aidha, Serikali itaendelea kutoa mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu katika mwaka wa fedha 2021/2022 bajeti iliyoongezeka kutoka bilion 464 hadi 570.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles