24.2 C
Dar es Salaam
Sunday, April 14, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa kuzindua kampeni kupinga ukatili

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi  katika uzinduzi wa maadhimisho ya kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili yatakayofanyika kitaifa Novemba 25,2021 kwenye ukumbi wa Mlimani City, jijini mkoani Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na  Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, Waziri Mkuu atazindua kampeni hiyo inayoongozwa na  kauli mbiu isemayo ‘Ewe Mwananchi Komesha Ukatili wa Kijinsia Sasa’ inayotoa jukumu kwa jamii kuchukua hatua madhubuti kama kizazi kinachoamini na kuthamini usawa wa kijinsia, kukomesha vitendo vya Ukatili wa Kijinsia katika maeneo yote hapa nchini.

“Kauli mbiu hii inatoa nafasi na majukumu kwa kila mtu katika nafasi yake kupaza sauti na kuchukua hatua ya kuzuia na kutokomeza vitendo vya ukatili” amesema Dk Gwajima. 

Amesema kupambana na tatizo la ukatili wa kijinsia, inabidi jamii kuunganisha nguvu zetu na kubuni mikakati ya kijamii ambayo ndiyo italeta suluhisho la kudumu. 

Dk. Gwajima ameeleza kuwa katika maeneo mengi ya nchi suala la uelewa kuhusu ukatili na madhara ya yake linafahamika na matokeo chanya yamepatikana kwa kuwashirikisha wananchi wenyewe na hasa kuwahusisha viongozi wa kijamii kama vile viongozi wa dini, kimila, wazee maarufu na watu wengi ambao wana sauti katika jamii husika. 

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima

Ameongeza kuwa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto ni suala lisilokubalika kimataifa na katika jamii yetu pia na mfano wa vitendo hivi vya ubakaji, ulawiti, vipigo, matusi, ukatili wa kingono na kunyimwa haki za kumiliki mali.

Amesema vitendo hivyo vinarudisha nyuma jitihada za Serikali katika kufikia usawa wa jinsia kwani waathirika wa ukatili hupata madhara makubwa ambayo hushusha hadhi na  ustawi wa mtu au familia inayofanyiwa ukatili.

Amefafanua kuwa kwa mujibu wa taarifa za Utafiti wa Afya ya Uzazi na Viashiria vya Malaria (TDHS-MIS 2015/2016) zinaonesha kwamba, asilimia 40 ya wanawake wa umri kati ya miaka 15-49 wamefanyiwa ukatili wa kimwili au kingono mara moja au zaidi katika kipindi chao cha maisha.

Aidha, asilimia 20 ya wanawake wa umri kati ya miaka 15-49 wamefanyiwa ukatili wa kimwili katika kipindi cha miezi 12 iliyopita, asilimia 9 ya wanawake wa umri kati ya miaka 15-49 wameingiliwa kimwili bila ridhaa yao.

Amesisitiza kuwa maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia yamelenga kuongeza nguvu za pamoja kama Taifa, kubadilishana taarifa na uzoefu, kuelimisha, kukemea na kuchukua hatua kwa pamoja ili kupinga aina zote  ukatili wa kijinsia katika jamii, kwa kuzingatia mazingira na matukio yanayoenda sambamba na kauli mbiu husika.

Dk. Gwajima amesema Serikali inaendelea kutekeleza mpango kazi wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto (2017/2018 -2021/2022).

Amesema Mpango huo, unalenga kupunguza kiwango cha ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika jamii yetu kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2022.

“Serikali kwa kushirikiana na wadau imeendelea kutoa huduma katika vituo 14 vya mkono kwa mkono nchini. Katika kipindi cha mwaka 2020/21, waathirika 1,857 wa ukatili wa kijinsia walipata huduma kati yao watoto 1,072 (wavulana 412 na wasichana 660) na wanawake 785,” amefafanua  Waziri Dk. Gwajima.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles