24.2 C
Dar es Salaam
Sunday, May 19, 2024

Contact us: [email protected]

MIAKA 60 YA AGA KHAN, UWEKEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO

Na MWANDISHI WETU- MWANZA

“TUNAMPONGEZA Prince Karim Aga Khan na taasisi zake zote kwa kuwekeza miradi mbalimbali ya maendeleo Tanzania. Kiongozi huyu ni mcha Mungu, anapenda kuona jamii inapata maendeleo, amani na upendo.”

Hii ni kauli ya Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Makanisa ya Mkoa wa Mwanza, Askofu Charles Sekelwa, aliyoitoa mbele ya kamati hiyo.

Hivi karibuni, kamati hiyo ilitembelea makumbusho ya Aga Khan yaliyopo Mwanza ikiwa ni maadhimisho ya kusherehekea miaka 60 ya uongozi wake.

Maadhimisho ya Uimamu wa Aga Khan yanakuja huku kiongozi huyo akiendelea kusifika duniani kutokana na dhamira yake ya kuiwezesha jamii kuwa na maisha bora.

Katika ziara hiyo, wajumbe wa kamati hiyo walijionea historia ya kiongozi huyo wa kiroho wa Madhehebu ya Kiislamu ya Shia Ismailia.

Pamoja na mambo mengine, viongozi wa kamati hiyo walieleza kufurahishwa na uongozi wake duniani.

Wenyeviti wa kamati hiyo, Sheikh Hassan Kabeke na mwenzake, Askofu Sekelwa, wanasema taasisi hiyo inastahili kuigwa na jamii yote ulimwenguni.

“Kwanza ziara yetu imetupa elimu kubwa. Tumejifunza namna ya kuwa kiongozi bora kwa waumini na kushiriki katika maendeleo.

“Mafanikio ya Aga Khan yanatokana na uongozi wake kupenda watu, amani na maendeleo ya nchi na mataifa,” anasema Sheikh Kabeke.

Viongozi hao wanasema uongozi wa Aga Khan, umetamalaki katika amani, upendo na maendeleo kwa jamii.

Wanasema taasisi na viongozi wote wa madhehebu ya dini hawana budi kuiga uongozi na uwekezaji miradi ya maendeleo unaofanywa na Aga Khan kwa jamii ulimwenguni.

Naye Katibu wa Baraza la Waislamu Mkoa wa Mwanza (Bakwata), Sheikh Mohamed Balla, alisisitiza suala la uwekezaji wa miradi hapa Tanzania.

“Tumeona Aga Khan anavyosaidia kuleta maendeleo katika nchi yetu. Jamii yote inapaswa kuiga mfano wa kiongozi huyo,” anasema.

AGA KHAN NI NANI?

Aga Khan alianza kuwa Imamu wa Madhehebu ya Kiislamu ya Shia Ismailia, Julai 11, 1957 akiwa kijana mwenye umri wa miaka 20.

Alichukua nafasi hiyo kubwa kiimani kutoka kwa babu yake, Sir Sultan Mohamed Shah Aga Khan.

Ni Imamu wa 49 wa madhehebu hayo. Inaelezwa ana nasaba ya moja kwa moja na Mtume Muhammad.

Tangu ashike nafasi hiyo, Aga Khan, amejielekeza katika ustawi wa Jumuiya ya Ismailia, Jumuiya ya Kiislamu kwa upana wake na jamii yote kwa ujumla.

Kiongozi huyu anasisitiza mtazamo wa Kiislamu ni kama fikra, imani ya kiroho inayofundisha huruma, uvumilivu na kutetea utu wa mtu.

Katika kizazi cha hivi karibuni, familia ya Aga Khan imekuwa ikishiriki kutoa huduma za kijamii katika nyanja mbalimbali za kimataifa.

Mfano, babu yake Aga Khan amewahi kuwa Rais wa League of Nations. Baba yake na Prince Aly Khan, amehudumu nafasi ya Balozi wa Pakistan katika Umoja wa Mataifa (UN).

Vivyo hivyo baba yake mdogo, marehemu Prince Sadruddin Aga Khan, alikuwa Mratibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR).

Alikuwa akisaidia Afghanistan na ujumbe wa UN katika mipaka ya nchi za Iraq na Uturuki.

Pia amekuwa akifanya kazi na Serikali tofauti kila moja ikiwa na matarajio yake. Aga Khan amekuwa akilinda, kutunza na kuzingatia siasa zisizoegemea upande wowote.

Amekuwa akiwekeza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini, ikiwamo sekta ya afya, elimu na masuala ya amani.

Maadhimisho hayo ya miaka 60 ya Aga Khan yanasherehekewa kwa muda wa mwaka mmoja kuanzia Julai 11, mwaka huu hadi Julai 11, mwakani.

Kwamba kiongozi huyo anatarajiwa kuzuru nchi 35 duniani, kisha kufungua na kuweka mawe ya msingi ya miradi mbalimbali ya maendeleo na atakutana na wanajumuiya ya Dini ya Ismailia kwa nchi hizo.

Pamoja na hayo, taasisi hiyo imejikita pia kuwekeza kwenye sekta ya elimu na imejenga shule mbalimbali za msingi na sekondari.

Taasisi hiyo ya Aga Khan inayomiliki shule mbalimbali hapa nchini ikiwamo ya Aga Khan Mzizima Sekondari pia kwa Zanzibar ina walimu 900.

UWEKEZAJI

Katika kusimamia misingi yake, Taasisi ya Maendeleo ya Aga Khan (AKDN) imejikita kusaidia upatikanaji wa maendeleo ya jamii kwa kuwekeza miradi ya afya na elimu nchini.

Kwa kutenga Dola milioni 15 za kuboresha hospitali za wilaya zilizopo mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Mpango huo umelenga kusaidia jamii kupata huduma bora zaidi za kiafya zikiwamo vipimo.

Taarifa ya Aga Khan inasema mbali na taasisi hiyo kuwa mdau mkubwa wa maendeleo duniani kote pia inahitaji kuona Watanzania wakiishi salama kiafya, kielimu, upendo na utulivu.

“Tayari tumefungua kituo cha afya Buzuruga Mwanza na Kahama Mkoa wa Shinyanga. Desemba, mwaka huu  tutafungua Tabora na Bukoba.

“Mwakani tutafungua pia huduma za afya Bunda mkoani Mara. Mwaka 2019 tutafungua Simiyu na Kigoma,” anasema Rais wa Aga Khan-Kanda ya Ziwa, Altaf Hiran Mansoor na kuongeza:

“Tayari programu hii ya maboresho ya hospitali za wilaya za Serikali, imeshafanyiwa tathmini.”

Chuo Kikuu

Katika kupigania maendeleo, Chuo Kikuu cha Aga Khan kinakusudia kujenga Chuo Kikuu cha Afya na Elimu kitakachokuwa cha pili duniani.

Chuo cha kwanza kama hicho kipo nchini Pakistan. Kitagharimu zaidi ya Dola milioni 300 za Marekani sawa na Sh bilioni 660.

Taratibu za ujenzi wake zinatarajiwa kuanza miezi sita ijayo kuanzia sasa. Kukamilika kwake kutabadili sura ya Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.

HOSPITALI

Mbali na chuo hicho, AKDN imekusudia kujenga hospitali kubwa kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Mansoor anasema hospitali hiyo itakayojengwa Mkoa wa Mwanza, itagharimu Dola milioni tano za Marekani sawa na Sh bilioni 12

“Hospitali yetu ya Dar es Salaam watu zaidi ya 4,000 wanatibiwa kwa gharama nafuu kila mwaka,” anasema Mansoor.

Baadhi ya wagonjwa wanaotibiwa Hospitali ya Aga Khan-Mwanza wanaeleza kufurahishwa na huduma bora zinazotolewa hospitalini hapo.

“Ukweli Hospitali ya Aga Khan ina huduma nzuri, bei zake nafuu na huduma ni bora,” anasema mkazi wa Mabatini, Mwanza, Asha Haruna.

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles