26.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, July 16, 2024

Contact us: [email protected]

Miaka 20 ya TCAA; yajivunia udhibiti maeneo ya usalama wa anga

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

MAMLAKA ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imesema kuwa wakati ikiadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwake imeweza kuimarika kwa uwezo wa udhibiti katika maeneo ya usalama wa anga pamoja na usimamizi wa wataalam wa usafiri wa anga ambapo katika kaguzi zilizofanywa na Shirika la Usafiri Duniani ufaulu wa Tanzania umekuwa ukiongezeka.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam leo Alhamisi Oktoba 5, na Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya maadhimisho ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo hapa nchini.

Alisema katika kaguzi hizo mwaka huu, mamlaka ilifaulu kwa asilimia 37.8, mwaka 2019, asilimia 69.04 na mwaka 2022, asilimia 86.7, alama hizo za ufaulu zinaifanya nchi kuaminika na hivyo kupelekea mashirika mbalimbali yanayotoa huduma za usafiri wa anga kuja kuwekeza nchini.

Alisema serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ya usafiri wa anga nchini ikiwa ni pamoja na upanuzi na ukarabati wa viwanja vya ndege vya Dodoma, Abeid Aman Karume, Mwanza, Iringa, Mtwara, Bukoba na hatimaye kuongeza uwezo wa kukidhi mahitaji yanayokua ya abiria na mizigo.

“Aidha Serikali inaendelea na ujenzi wa uwanja mpya wa ndege wa Msalato jijini Dodoma ambao ukikamilika utaongeza idadi ya viwanja vya kimataifa, uboreshaji huu wa miundombinu sio tu kwamba umeimarisha mawasiliano ndani ya Tanzania lakini pia umeiweka nchi kama kitovu cha usafiri wa anga kikanda,” amesema Hamza.

Mbali na mafanikio hayo amesema TCAA inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa wataalamu wenye ujuzi katika sekta ya usafiri wa anga.

Aidha alisema mamlaka hiyo inakabiliwa pia na uchakavu wa mitambo ya kuongozea ndege na miundombinu duni ya usafiri wa anga nchini kama viwanja vya ndege na mifumo ya mawasiliano.

Johari amesema sekta hiyo ya usafiri wa anga inakuwa kwa kasi lakini ongezeko la wataalamu ni ndogo na haliendani na kasi hiyo hivyo mamlaka hiyo imeendelea kujipanga ili kuhakikisha wanaongeza idadi ya wataalamu.

“Tuna upungufu wa wahandisi wa ndege ila zaidi kabisa marubani, sasa hivi tuna idadi ya marubani 603 lakini kulingana na mahitaji ya soko, ukuaji na ndege zinavyoongezeka kununuliwa tunatakiwa kuwa na marubani zaidi ya 780, hata hivyo inachojua kuwa tuna upungufu wa takribani marubani 150 ili kuweza kuendana na ukuaji wa soko,” amesema na kuongeza:

“Katika kukabiliana na changamoto hiyo tumeanzisha mfuko wa marubani, umeanzishwa kwa mujibu wa sheria ambapo wadau wote kwenye usafiri wa anga wanachangia, tukizipata fedha hizo tunatangaza nafasi kwa wanafunzi waliosomea sayansi waje kuomba na tunawachukua kisha tunawasomesha urubani nje ya nchi, mpaka sasa tumeshasomesha marubani 22 wakiwemo wanawake nane na wanaume 14,” amesema.

Aidha, alisema pia wanakabiliwa na changamoto ya kuathirika kwa uwezo wa kifedha wa mamlaka uliotokana na kudorora kwa biashara ya usafiri wa anga baada ya mlipuko wa Uviko 19.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles