Johns Njozi, Dar es Salaam
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imeanza kutumia mfumo wa kielektroniki wa kutunza taarifa za mawakili kuhusu usajili na sifa zao kwa lengo la kudhibiti mawakili vishoka na wanaofanya kazi bila kuwa na leseni
Kwa mujibu wa taarifa ya Msajili wa Mahakama Kuu, mfumo huo kwa sasa uko tayari kwa matumizi ya umma ambapo mtu anaweza kuthibitisha iwapo wakili wake anafanya kazi kihalali au la.
Taarifa hiyo pia imeeleza ni kosa kwa wakili kufanya kazi bila kuwa na leseni ya uwakili na iwapo atafanya hivyo uwakilishi wake Mahakamani au kazi yoyote aliyoifanya ni batili.
“Unaweza kutambua kama wakili wako anafanya kazi kihalali kupitia tovuti rasmi ya mahakama ambapo kama wakili ana leseni hai ya uwakili itatokea picha yake katika rangi ya bluu ikiambatana na maneno ‘anaruhusiwa’ na kama hana leseni itaandika ‘haruhusiwi’ na picha yake itakuwa katika rangi nyekundu,” imesema taarifa hiyo.
Aidha, mfumo huo ambao unatumia lugha ya Kiswahili na Kiingereza kama lugha rasmi, unasema endapo picha ya wakili inaonyesha haruhusiwi, si sahihi kufanya naye kazi za kisheria au biashara yoyote.