30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Meya amwaga ‘mapesa’ Dar

Boniface-JacobNA KOKU DAVID

MEYA wa Manispaa ya Kinondoni,  Boniface Jacob, amesema wametenga kiasi cha shilingi bilioni 4.5 kwa mwaka wa fedha 2015/2016 kwa ajili ya kuwasaidia kiuchumi wanawake na vijana wa Manispaa hiyo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa kukabidhi sehemu ya fedha hizo, Jacob alisema hadi kuwafikia walengwa  zitatolewa kupitia Benki ya Wananchi Mkoa wa Dar es Salaam (DCB).

Alisema fedha hizo ni asilimia 10 ya mapato yote ya ndani ya Manispaa hiyo ambayo inatakiwa kutoa kwa ajili ya kuwawezesha wanawake na vijana katika shughuli zao za kiuchumi.

Alisema jana amekabidhi Sh 19,500,000 kwa vikundi sita na kwamba zoezi hilo la ugawaji wa fedha za mkopo kwa ajili ya kujikwamua kimaisha litakuwa endelevu ili kutekeleza agizo la Serikali.

“Ndugu wananchi fedha zipo kwa ajili yenu naomba mchangamkie fursa kwani ni mkopo ambao hauna masharti magumu na riba yake ni asilimia 10 tu ambayo ni rahisi kuliko benki zote,” alisema Jacob.

Alisema fedha hizo ni za awamu ya kwanza na kwamba katika awamu ya pili wanatarajia kutoa Sh bilioni 5.5 ambazo zitatokana na bajeti ya mwaka wa fedha wa 2016/2017.

Jacob alizitaja baadhi ya kata alizozikabidhi hundi kwa ajili ya mikopo na kiasi cha fedha kwenye mabano kuwa ni Kata ya Kigogo (7,700,000), Kata ya Kilungule B (3,000,000), Kata ya Saranga Mtaa wa Kimara B (4,100,000), Kata ya Saranga Mtaa wa Stop Over (2,100,000), Kata ya Goba Mtaa wa Goba (2,650,000) na Kata ya Goba Mtaa wa Mwembe Dole.

Naye Meneja Mikopo wa benki ya DCB, Maria Kabeho, alisema wahitaji wote wanatakiwa kujiunga katika kikundi cha watu watano ili waweze kupatiwa mkopo.

“Tunachotaka sisi ni uaminifu na uthubutu wa vikundi ili tuweze kuwapatia mikopo,” alisema Maria.

Kwa upande wake, Emmanuel Abdul ambaye ni kiongozi wa madereva wa bodaboda katika Kata ya Goba Mtaa wa Goba, alisema mkopo huo utawasaidia kutanua mitaji yao na kwamba wanaomba mikopo hiyo iwe endelevu.

Pia alisema wanaomba wasaidiwe wawe wanafika mjini kupeleka abiria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles