27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, June 13, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yaapa kufyeka ufisadi  

Kassim MajaliwaNA BAKARI KIMWANGA, DODOMA

SERIKALI imetoa kauli ya kiapo bungeni kuwa itapambana hadi iviangamize vitendo vyote vya rushwa na ufisadi vinavyofanywa na watumishi wa umma wasio waaminifu.

Imesema sambamba na hilo pia itaendelea kuisafisha Mamlaka ya Bandari (TPA) na imewataka wafanyabiashara watambue kuwa ipo na inaendelea kuboresha huduma katika bandari zote hususani ya Dar es Salaam.

Kauli hiyo imetolewa bungeni jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alipokuwa akiwasilisha bajeti ya Sh bilioni 236.75 kwa ajili ya ofisi yake.

Katika hotuba yake hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa alisema Serikali inaendelea vizuri na utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Rais John Magufuli wakati wa uzinduzi wa Bunge la 11, Novemba 20, mwaka jana ya kuanzisha Mahakama maalumu ya ufisadi.

Alisema tayari Serikali imekwishaanzisha Divisheni ya Mahakama ya Rushwa na Ufisadi katika Mahakama Kuu inayotarajiwa kuanza kufanya kazi Julai mwaka huu.

“Napenda kuliarifu Bunge kuwa Serikali itaendelea kupambana na rushwa kwa kuchunguza tuhuma na kuwafikisha watuhumiwa mahakamani. Serikali itaimarisha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kwa pamoja ziweze kuharakisha utoaji haki,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Akizungumzia mwenendo wa mapambano ya rushwa, alisema katika kipindi cha mwaka 2015/2016, Serikali imeshughulikia tuhuma za rushwa 3,911 huku uchunguzi wa tuhuma 324 ukikamilika na kati ya hizo, majalada 252 yaliombewa kibali cha mashtaka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ambapo majalada 156 yalipata kibali.

Alisema majalada 329 yaliyotokana na taarifa ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na 19 kati ya hayo yalikamilika na kuombewa kibali cha mashtaka kwa DPP ambaye aliidhinisha majalada ya watuhumiwa 12 kufikishwa mahakamani.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema sambamba na hatua hizo, Serikali inaendelea kuwaondoa katika utumishi wa umma wafanyakazi wasiokuwa waaminifu wanaoisababishia hasara kwa kuipotezea mapato.

Aidha, alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuboresha huduma katika bandari zote ili kupunguza idadi ya siku za kutoa mizigo bandarini hadi kufikia mbili au chini ya hapo.

“Tutaziondoa kero zote zilizoainishwa na Mawakala wa Forodha nilipokutana nao tarehe 21 Machi, 2016 jijini Dar es Salaam. Vile vile, Serikali itaziba mianya yote ya upotevu wa mapato bandarini na wale wote watakaobainika kushiriki kwenye wizi wa aina yoyote wataondolewa na kuchukuliwa hatua za kisheria,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Katika hotuba yake hiyo ya kuwasilisha bajeti ya ofisi yake na taasisi zake kwa mwaka 2016/2017 ambapo aliliomba Bunge liidhinishe jumla ya Sh 236,759,874,706, alisema makadirio ya bajeti aliyoyafikisha bungeni ni mwendelezo wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 inayoainisha ahadi za Serikali kwa miaka mitano.

“Makadirio ya bajeti yamezingatia ahadi za Rais John Magufuli, alizotoa wakati wa kampeni na katika uzinduzi wa Bunge la 11, Nevomba 20, mwaka jana kuhusu kufikia malengo yaliyokusudiwa ya kujenga taifa imara kiuchumi na maendeleo ya watu katika Kanda ya Afrika Mashariki na barani Afrika kwa ujumla,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Kabla ya kuhitimisha hotuba yake, Waziri Mkuu Majaliwa alieleza kushangazwa na mwitikio mdogo wa wapigakura katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Alisema pamoja na kazi nzuri iliyofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na wananchi kuitikia wito wa kujiandikisha na kupiga kura, idadi kubwa ya waliojiandikisha hawakujitokeza.

“Naiagiza Tume ya Uchaguzi kufanya tathmini ya kina kubaini sababu zilizofanya wapiga kura zaidi ya milioni saba waliojiandikisha kupiga kura kutoitumia haki yao ya Kikatiba. Hii itasaidia kuboresha chaguzi zijazo kwani wananchi wana wajibu wa kutumia haki yao ya msingi kuchagua viongozi wanaowataka.

“Tathmini itasaidia kubaini iwapo kuna vikwazo vinavyowazuia baadhi ya watu kupiga kura ili kwa pamoja tuviondoe.

“Ndani ya Bunge hili tupo wabunge wa vyama mbalimbali lakini kwa lengo moja tu la kuwawakilisha wananchi wetu na kuishauri Serikali ili ipange mipango mizuri itakayoharakisha maendeleo yao.

“Niseme tu kwamba sasa Uchaguzi Mkuu umekwisha na Serikali zetu zipo madarakani kwa mujibu wa Katiba. Hivyo, tuienzi falsafa ya Rais ya “Hapa Kazi Tu!” kwa kuchapa kazi na tusitoe nafasi kwa tofauti zetu za kisiasa na kiitikadi kuwa kisingizio cha kukwamisha shughuli za maendeleo ya nchi yetu,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Wakati huo huo, kiongozi huyo wa shughuli za Serikali bungeni amewaagiza wakuu wa mikoa na wilaya kupambana na changamoto ya upungufu wa madawati baada ya kuanza kuandikisha watoto shule bila malipo.

“Kuanzia leo hii (jana), nawaagiza wakuu wa wilaya na wakurugenzi waliokamata mbao ndani ya Halmashauri zao kuzitumia kutengenezea madawati na siyo kuzipiga mnada. Natumia nafasi hii kukushukuru wewe Mheshimiwa Spika na Watendaji wa Bunge kwa Mkakati wa kubana matumizi uliowezesha kupata shilingi bilioni sita zitakazotumika kutengeneza madawati.

“SUMA JKT na Magereza wameanza kazi ya kutengeneza madawati hayo. Tunatarajia kupata madawati 80,000 ambayo tutawagawia wabunge wa majimbo yote na kwa wastani kila jimbo litaweza kupata madawati 300,” alisema.

Ukuaji wa uchumi

Akizungumzia sekta ya uchumi, Waziri Mkuu Majaliwa, alisema malengo ya Serikali ni kufikia nchi ya kipato cha kati na kufanya mapinduzi makubwa ya viwanda ambayo yanategemea utulivu wa uchumi.

Alisema kwa ujumla ukuaji wa uchumi umekuwa wa kuridhisha kwani mwaka 2015, uchumi ulikua kwa asilimia 7.1 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 7.0 mwaka 2014.

Alizitaja sekta zilizochangia ukuaji huo kuwa ni ujenzi, mawasiliano, fedha, uchukuzi na nishati.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles