29.3 C
Dar es Salaam
Thursday, June 1, 2023

Contact us: [email protected]

Muhimbili yafafanua matibabu ya sickle cell

NA JOHANES RESPICHIUS, DAR ES SALAAM

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH), imetoa ufafanuzi kuhusu utaratibu mpya wa matibabu kwa wagonjwa wa selimundu (sickle cell) baada ya kumalizika kwa ufadhili wa mradi wa  matibabu hayo.

Imesema huduma ya matibabu ya wagonjwa wa selimundu bado inatolewa hospitalini hapo ambapo sasa wataingizwa kwenye mfumo wa kawaida wa matibabu.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa MNH, Aminiel Aligaesha, alieleza kuwa hospitali hiyo haijasitisha utoaji wa huduma kwa wagonjwa wa selimundu tofauti na ilivyoripotiwa awali.

“Ni kweli kwamba takribani miaka kumi iliyopita kulikuwa na mradi uliokuwa ukifadhili matibabu pamoja na utafiti wa wagonjwa wa selimundu ambao muda wake umeisha Machi 31 mwaka huu, hivyo basi hali hii ilisababisha wagonjwa wengi wanaohitaji huduma ya selimundu kuja hospitalini hapa licha ya kwamba mahitaji yao hayakuhitaji wataalamu,” alisema Aligaesha.

Alisema kabla ya mradi huo, MNH ilikuwa inatibu wagonjwa hao na walikuwa wanapatiwa rufaa kulingana na maradhi yao kutoka hospitali za mikoa.

Wakati MNH ikitoa taarifa hiyo, mwanaharakati mwenye mtoto anayeumwa selimundu aliyejitambulisha kwa jina la Yasmin Razak, amelieleza gazeti hili kuwa mabadiliko ya matibabu hayo yamekuja bila kutolewa taarifa yoyote.

Alisema kuwa tangu Novemba mwaka jana Muhimbili walitumiwa barua kwamba mradi huo unaisha Machi mwaka huu hivyo watafute namna ya kuwahudumia wagonjwa hao lakini jambo la kusikitisha hawakutoa majibu yoyote.

“Hawakutoa majibu wala kutuma barua mikoani kuwa wagonjwa hao watakuwa discharged huko na baada ya mradi kuisha Muhimbili waliwaambia zaidi ya wagonjwa 700 kuacha kwenda kupata matibabu hayo ya bure,” alisema Razak.

Alisema mradi huo ulikuwa unahudumia bure watu wote wenye mahitaji ya matibabu hayo wapatao 6,000 na kwamba Muhimbili walitoa jengo ambalo lilikuwa likilipiwa Dola za Marekani 2,000 sawa na Sh 4,401,200 za Tanzania pamoja na kuajiri madaktari.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya Temeke, Dk. Amani Malima, alisema katika hospitali hiyo kuna kliniki ya kawaida kwa watoto na watu wazima wenye ugonjwa wa selimundu.

Alisema kulingana na sera ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, matibabu ya wagonjwa wa selimundu hutolewa bure lakini ukosefu wa baadhi ya vifaa inalazimu kulipiwa.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Grace Magembe, alisema hakuna barua aliyopokea MNH ya kusitishwa kwa matibabu ya bure kwa wagonjwa wa selimundu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,225FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles