Na KULWA MZEE-DAR ES SALAAM |
ALIYEKUWA Mbunge wa Dimani, Zanzibar, Abdallah Sharia (CCM) na mwenzake, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu  wakidaiwa kufanya udanganyifu na kujipatia Sh milioni 55.
Mshtakiwa Sharia na Dk. Athuman Rajabu walifikishwa mahakamani   jana na kusomewa shtaka lao mbele ya Hakimu Mkazi Hamis Ally.
Akisoma mashtaka, Wakili wa Serikali, Janeth Magoho alidai washtakiwa hao walitenda kosa hilo kati ya Julai 17 na Septemba 29, 2017, Dar es Salaam.
Washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kwa nia ya udanganyifu walijipatia kutoka kwa Dk. Abdi Hirsi Warsame, Â Sh milioni 55 baada ya kumdanganya kwamba wangemsambazia vifaa tiba vya hospitali.
Washtakiwa   walikana shtaka hilo, Upande wa Jamhuri ulidai upelelezi haujakamilika na waliomba kuahirisha kesi hiyo hadi tarehe nyingine ya kutajwa.
Wakili wa utetezi, Timotheo Wandiba, Â aliomba washtakiwa wapatiwe dhamana kwa kuwa shtaka linalowakabili linadhaminika.
Hakimu Ally alitoa masharti ya dhamana yaliyomtaka kila mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili watakaotia saini dhamana ya maandishi ya Sh milioni 27.5.
Pia kila mshtakiwa kuwasilisha hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh milioni 27.5 na Wakili Wandiba aliomba kesi hiyo iahirishwe hadi leo kwa kuwa wadhamini walikuwa hawajakamilika.
Washtakiwa hao walipelekwa mahabusu hadi leo  kwa ajili ya kutimiza masharti ya dhamana.