Derick Milton, Simiyu
Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Simiyu, Leah Komanya (CCM) amekabidhi vifaa mbalimbali vyenye thamani ya Sh milioni 17 kwa ajili ya matumizi ya ofisi za Chama Cha Mapinduzi kila wilaya mkoani humo ili kurahisisha utendaji kazi za chama.
Vifaa hivyo ni pamoja na mashine tano za kudurufu, wino, vifaa vya kudhibiti umeme na mashuka 200 kwa vituo vya afya viwili kila wilaya.
Akikabidhi vifaa hivyo leo Ijumaa Aprili 17, mbunge huyo amesema wilaya zote tano zimepatiwa mashine moja, wino mmoja, na kifaa kimoja cha umeme, ambapo vitatumiwa na ofisi za chama hicho na jumuiya zake.
Amesema ameamua kuleta vifaa hivyo baada ya kuona jinsi ofisi za chama hicho mkoani humo zinavyohangaika katika kudurufu kazi za chama.
“Niliona kama changamoto kubwa sana ambayo ilikuwa inatukabili, ilisbabisha hadi siri za chama kutoka nje ya ofisi kwa urahisi jambo ambalo siyo jema, kwa vifaa hivi najua changamoto hii haitakuwapo tena,” amesema Komanya.
Akipokea kwa niaba ya chama hicho, Katibu Mkuu wa CCM Mkoa, Haula Kachwamba amesema kuwa msaada huo umekuja wakati mwafaka kwani ndiyo kipindi cha kudurufu kazi nyingi za chama kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Kwachwamba amesema kuwa Mbunge huyo amekuwa mbunifu na amempongeza kwa kufikiria kuleta mashine hizo, ambazo alisema zitaondoa tatizo la kutanga tanga mitaani kudurufu kazi cha chama.