Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe, amezindua Programu (WanaNzengo Airtel FURSA) jimboni kwake ambayo itawawezesha zaidi ya wajasiriamali 350 kunufaika na mikopo kupitia huduma ya Airtel Money.
Mikopo hiyo itatolewa kwa kikundi kilichoundwa na vijana watano ambao watapewa mtaji kati ya shilingi Shs.100,000 hadi 1,000,000 kulingana na mahitaji yao.
Sambamba na mikopo ya vikundi vya wajasiriamali vitapewa mafunzo ya ujasiriamali ikiwa ni pamoja na namna ya kuendesha vikundi pamoja na jinsi ya kutafuta soko, kusimamia mahesabu na nyenzo muhimu zitakazowapatia mafanikio katika biashara zao.
“Nawapongeza sana Airtel Tanzania kwa kuungana nasi katika kutekeleza juhudi zetu za kuhakikisha tunainua uchumi mdogomdogo na kuwawezesha wajasiriamali kuwa na mitaji tena isiyo na riba kubwa na yenye masharti nafuu kabisa itakayowasaidia kukuza kipato chao,” alisema Bashe
Aliongeza kwakusema, “Tumejipanga kuhakikisha kiasi hiki cha shilingi millioni 20 kilichotolewa na Airtel kinatumika vyema ili kuweza kuwafikia wajasiriamali wengi zaidi, pesa hizi zitazunguka mikononi mwa wajasiriamali na hivyo tunahimiza vikundi vitakavyokopa viweze kurejesha mikopo yao kwa wakati bila usumbufu ili wengi waweze kufaidika na programu hii,”.
Pamoja na mambo mengine, Bashe aliwahimiza vijana kujiunga na vikundi vya ujasiriamali kuepusha wimbi la ukosefu wa ajira nchini na kuacha tabia ya kushiriki katika vitendo viovu ambavyo vinahatarisha maisha yao na usalama wa taifa kwa ujumla.
Pia alisisitiza kuwa maelezo ya jinsi ya kushiriki nitayaweka katika ukurasa wangu, website yangu pamoja na ofisi ya Mbunge jimboni Nzega.