Na MOHAMED KASSARA
TIMU ya Taifa Tanzania ‘Taifa Stars’, imejikuta ikiangukia pua na kukubali kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Cape Verde katika mchezo wa kusaka tiketi ya kushiriki fainali za Mataifa Afrika (Afcon) uliochezwa juzi Uwanja wa Taifa, jijini Praia.
Kipigo hicho kimezidi kufifisha ndoto ya Tanzania kufuzu fainali za Afcon zitakazofanyika mwakani nchini Cameroon.
Stars itarudiana na Cape Verde keshokutwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Stars itaingia katika mchezo huo, ikiwa haina cha kupoteza kwani itahitaji kushambulia zaidi ili kupata ushindi wa kuiweka pazuri katika msimamo wa kundi lake.
Matokeo hayo yaliifanya Stars kushika nafasi ya mwisho katika msimamo wa kundi L, ikiwa na pointi mbili, huku Cape Verde ikifikisha pointi nne na kupanda hadi nafasi ya pili.
Stars tayari imecheza michezo mitatu bila kupata ushindi, ikianza kwa sare ya bao 1-1 na Lesotho, Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, suluhu dhidi ya Uganda, Uwanja wa Nelson Mandela jijini Kampala, kabla ya juzi kuchapwa mabao 3-0 na Cape Verde.
Hadi sasa kikosi cha Stars ndicho kilichoruhusu mabao mengi katika kundi hilo, ambapo imepigwa mabao manne huku yenyewe ikifunga bao moja.
Kwa maana hiyo, Stars itahitaji kushinda michezo yake mitatu iliyosalia kwenye kundi hilo ili kufufua upya matumaini ya kufuzu kwa fainali hizo ambazo kwa mara ya mwisho ilishiriki mwaka 1980.
Ilipoangukia Stars
Katika mchezo wa juzi, Stars iliangushwa na mambo mengi lakini kubwa ni plani ya mchezo na kukosekana kwa umakini.
Kocha Mkuu wa Stars, Emmanuel Amunike, aliamua kuingia na mpango wa kujilinda zaidi na kushambulia kwa tahadhari ili kupata angalau pointi moja katika mchezo huo.
Mpango huo ulilenga kuhakikisha timu yake inapata ushindi kupitia mashambulizi ya kushtukiza, lakini kama hawatafanikiwa basi wasipoteze mchezo.
Amunike aliingia na mpango huo kwa kuwa alikuwa ugenini.
Mfumo huo ulimsaidia kuanza kazi yake vizuri kwa kupata pointi moja katika mchezo mgumu dhidi ya Uganda.
Kocha huyo raia wa Nigeria, alianzisha kikosi kile kile kilichompa pointi moja kule Uganda.
Lakini kutokana na kutowafahamu vizuri wachezaji wa timu pinzani katika mchezo wa juzi, plani yake ilijikuta ikishindwa kumpa matokeo chanya.
Mpango huo wa kujilinda ulifanikiwa katika mchezo wa awali kutokana na wachezaji wa Tanzania na Uganda kufahamiana hivyo ilikuwa rahisi kuwadhibiti wapinzani hao.
Katika mchezo dhidi ya Cape Verde, kikosi cha Stars kilikuwa na sura mpya moja. Waliosalia walikuwa wale wale walioanza dhidi ya Uganda.
Katika mchezo huo alikosekana kiungo, Frank Domayo, ambaye nafasi yake ilizibwa na Himid Mao.
Ukiangalia mchezo uliopita, Stars japo ilijilinda lakini ilikuwa inamiliki mpira na kutengeneza mashambulizi kuelekea lango la Uganda, tofauti na ilivyokuwa Cape Verde.
Katika mchezo wa Cape Verde ilicheza kwa tahadhari ya juu hali iliyowapa mwaya Cape kutawala maeneo yote na kutengeneza mashambulizi yaliyowapa mabao mawili ya haraka.
Hii inaonyesha Amunike na benchi lake hawakupata muda wa kutosha kuitazama Cape Verde, ndiyo maana aliingia na mpango huo kutokana na kuiheshimu zaidi.
Kitaalamu unapokuwa unawapa nafasi wapinzani wako kukaa na mpira kwa muda mrefu unatoa nafasi pia kwako kupoteza umakini hivyo kufanya makosa, kwa vile muda mwingi utakuwa unakimbia kuutafuta mpira.
Hili lilidhihirika pale Stars ilipofungwa bao la kwanza, ambapo mfungaji aligusa mpira mara kadhaa kabla ya kufunga bila mabeki watatu wa Stars kuondoa mpira huo katika eneo la hatari.
Stars ilikuwa na wachezaji wengi kwenye eneo lao la ulinzi, lakini walikuwa wanakosa umakini na kuruhusu wapinzani wao kupenyeza mipira iliyokuwa na madhara.
Mfumo wa kujilinda uliwanyima uhuru Mbwana Samatta na Simon Msuva, kusukuma mashambulizi langoni mwa Cape Verde kutokana na kukosa mipira kutoka kwa viungo ambao walikuwa bize kukaba.
Hali hiyo ilimfanya Samatta kutokuwa na madhara kwenye lango la Cape Verde kwa kuwa alikuwa analazimika kushuka chini kwenda kuchukua mpira na kutumia nguvu nyingi kuisogeza mbele, lakini hata hivyo alikuwa akikosa msaada kutoka kwa Msuva na Thomas Ulimwengu.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Amunike alikiri wachezaji wake walikosa umakini na kuruhusu bao rahisi dakika 20 za mwanzo.
“Tulipoteza mchezo katika kipindi cha kwanza kwa sababu tulishindwa kutimiza majukumu yetu kama timu, naamini bado tuna nafasi ya kujisahihisha katika mchezo ujao nyumbani, kundi bado liko wazi, kwa kuwa tukishinda Jumanne tutafikisha pointi tano, inaumiza kupoteza, lakini tunapaswa kujifunza kutokana na makosa,” alisema.