Na MWANDISHI WETU,
“MWONGOZO mpya wa maadili unapaswa kuigwa na jamii ili kulinda haki za wanawake na wasichana dhidi ya vitendo vya ukandamizaji wa kijinsia unaoendelea dhidi yao ndani ya jamii ya Kitanzania.”
Kauli hii imetolewa na Mtaalamu wa masuala ya sheria, Jamal Omary wakati akifanya mahojiano na gazeti hili.
Anasema; “nchi inapaswa kubadili mwenendo wake wa kukabiliana na masuala ya ubakaji, ulawiti na mateso ya aina yoyote yale dhidi ya wanawake.”
Anasema kuwa inaonekana kwamba mikakati ya kitaifa ya kupambana na maovu kama haya yameshindwa na hivyo Taifa linapaswa kutumia njia mbadala ili kuzuia ama kukomesha kabisa matatizo haya.
Maoni ya mtaalamu huyu yanajitokeza wakati ambapo matokeo ya ubaguzi na ukiukwaji wa haki za binadamu unaowalenga wanawake pamoja na
wasichana unaongezeka katika maeneo ya mjini na vijijini hapa nchini.
Kwa mujibu wa ripoti za hivi karibuni zilizotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), ubakaji na vitendo vya ulawiti umeongezeka kutoka 1,585 na kufika 1,765 kati ya mwaka jana na mwaka
huu.
Ingawaje ripoti imeonyesha kuwapo kwa ongezeko kubwa la vitendo vya ulawiti na ubakaji dhidi ya wanawake na wanaume, uwiano wa uchambuzi
wa ripoti hii unaonyesha kuwa zaidi ya watu 1,200,000 wameripotiwa kulawitiwa wakati wa kipindi hicho.
“Tarakimu hizi zinaweza kuwa juu kwa kuwa waathirika wengi wa majanga haya hawaripoti polisi pindi wanapopatwa na matatizo,” vyombo
vya habari vilimnukuu Mkurugenzi Mkuu wa LHRC, Dk. Hellen Kijo Bisimba akisema kwa kutumia taarifa za takwimu
zilizokusanywa na polisi kitengo cha jinsia hapa nchini.
Matokeo ya utafiti wa kipekee unaonyesha kuwa kumekuwapo na ongezeko la ghafla la idadi ya waathirika wa kubakwa, mateso ya kijinsia na kutekwa nyara kwa wasichana hapa Tanzania.
Uchunguzi uliofanywa wa kisayansi na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake nchini (TAMWA) pamoja na baadhi ya taasisi za haki za binadamu zinaonyesha kuwa Zanzibar inaongoza kwa matukio ya ubakaji inayowahusu wasichana.
Mimba za utotoni pamoja na kuolewa wakiwa na umri mdogo haya yote hayaripotiwi ipasavyo kwenye vyombo mahususi vya kusimamia sheria nchini.
“Nikwambie kitu, hapa Zanzibar kumbaka msichana ni jambo la kawaida, hii ni sehemu ya utamaduni wa watu wa mwambao wa pwani. Unaweza
kukuta taarifa kama hizi kwenye familia nyingi na cha kushangaza ni kwamba hakuna mtu anayethubutu kuripoti hizi taarifa kituo cha polisi,” anasema mkazi mmoja wa Kijiji cha Kinzikazi kilichopo Mkoa wa kusini Unguja.
Naye NashonMsangi, ambaye ni mratibu wa sheria anayeishi Kibaha, anasema wanawake wamekuwa wakishurutishwa katika maovu mengi yanayovunja haki zao za msingi kuanzia chini hadi kufikia ngazi ya Taifa.
Kwa muda mrefu sasa juhudi za watetea haki za wanawake na binadamu pamoja na taasisi zinazofanya kazi kwa niaba ya serikali hawajaweza kufaulu kurekebisha hali hiyo.
“Hata hivyo, wahusika wakuu wa mambo haya ndani ya jamiii yetu bado hawajatiwa nguvuni ukizingatia kwanba uchunguzi wa kipolisi na upelelezi unachukua muda mrefu zaidi ya mwaka,” anasema na kuongeza kuwa polisi wanapaswa kuongeza juhudi zao ili kuwabana wahusika wa matukio haya.
Takwimu zinaonyesha kuwa mmoja kati ya wasichana watatu wenye umri usiozidi miaka 18 wamewahi kupatwa na mikasa ya kubakwa, hii ni kwa
mujibu wa takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Watoto (UNICEF).
Hivi majuzi, vyombo vya habari vya ndani vilikariri ripoti ilitolewa na Tamwa ikiitaka serikali kuchukua hatua madhubuti kupambana na suala hili ikiwamo kuwapeleka mahakamani wahusika.
“Kama vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wizara husika italisimamia suala hili kwa usahihi kabisa na kuchukua hatua stahiki dhidi ya wahusika wanaodhalilisha utu wa watoto na wanawake kwa ujumla, nchi itakuwa ya amani kuishi,” inasema sehemu ya taarifa ya Tamwa.
Hata hivyo, katika kushughulikia masuala haya jamii inahitaji kuwa na mtazamo mpya ili kutokomeza kabisa unyanyasaji huu wa kijinsia na aina
yoyote ile ya unyanyasaji unaolengwa kwa wanawake na wasichana hapa nchini.
“Unaweza kuniamini au la, lakini ukweli wa suala hili unabakia kwamba ulinzi wa kijamii na kisheria dhidi ya wanawake na wasichana nchini umeshindwa kuleta matokeo mema yaliyotarajiwa.
“Hakika tunahitaji kubadilika,” anasema Fortunata Kitokesya ambaye ni Ofisa wa Programu ya Masuala ya akina mama katika taasisi ya kutoa huduma za kisheria ijulikanayo kwa kifupi LSF. Taasisi hii pia inatoa huduma za kifedha na masuala ya kitaalamu kwa mashirika yanayojihusisha na utoaji wa huduma za kisheria kwa wananchi.
“Wanawake na wasichana wameteseka kwa kipindi kirefu mno na wataendelea kuteseka kama hatua madhubuti hazitachukuliwa ili suala
hili likomeshwe, jamiii inabidi ibadilishe mikakati,” anasema.
Anasema kuwa LSF imeamua kuweka nguvu za kisheria katika mkakati wa juu wa kimaadili, ambao anaamini utawaokoa mamilioni ya wanawake na wasichana wanaoathirika na kupanuka kwa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu.
Dhana ya nguvu ya kisheria inatoa hamasa ili kuiwezesha jamii mbalimbali wakiwamo viongozi wa dini kwa minajiri ya kuwafanya waelewe dhana halisi ya haki za wanawake kama vile kumiliki ardhi, urithi, huduma za jamii ili waendeshe maisha bora.
Kwa kuzingatia dhana ya nguvu kisheria, Ofisa wa LSF anasema jamii na viongozi wa familia wataelimishwa na kuhamasishwa kuheshimu haki za msingi za wanawake na wasichana na kwamba kupitia mpango huu jamii itaelimishwa jinsi ya kupambana na mimba za utotoni, maovu kama ya unyanyasaji, ubakaji na mengine mengi.
“Baada ya kuelimishwa na kuzielewa dhana zote hizi, viongozi hawa wataweza kuwaeleza wananchi wao kusitisha maovu yao ya nyuma. “Kwa kweli ni vigumu kubadilisha mwenendo wa watu kupitia taarifa za kusomwa ama maelekezo yanayotolewa na viongozi wa kitaifa,” anasema.
“Tunatoa elimu kwa viongozi na ambao wanapoaswa kuisambaza kwa wananchi wao. Huu ndio mfumo thabiti na njia iliyosahihi ya kupambana na unyanyasaji wa kijinsia unaoendelea dhidi ya wanawake ili kuwahakikishia ulinzi madhubuti hapa nchini,” anaongeza Kitokesya.
Mwaka 2014, LSF ilijikita katika suala la uhamasishaji wa nguvu ya kisheria katika kulinda haki za wanawake na wasichana na kuanzisha miradi mitatu ya mwanzo kwenye miji ya Mvomero, Morogoro, Dar es Salaam na Siha, Kilimanjaro.
Katika kuitekeleza, taasisi ya TSF ilianzisha mawakala wa kubadili mtazamo huu ambao walizunguka huku na kule wakielimisha wananchi ndani
ya jamii zao jinsi ya kuheshimu na kulinda haki za wanawake na wasichana na kusitisha ubaguzi dhidi ya makundi ya kijamii isiyokuwa na uwezo.
“Katika dhana nzima ya kubadilisha tabia, mwenendo na mtazamo wa watu dhidi ya wanawake kuanzia ngazi ya chini kabisa unaweza kuleta sura
mpya tofauti ndani ya jamii ya Tanzania na kutafsiri mabadiliko ya mtazamo wa viongozi wa kitaifa na mawaziri wa serikali bila kutumia nguvu yoyote ile.
LSF pia inashughulika na maadili kama haya kwenye miradi yake inayetekelezwa sehemu mbalimbali katika wilaya 158 iliyopo hapa Tanzania. Maadili haya yamewaleta pamoja wanasheria, viongozi wa jamii katika kueneza masuala ya wanawake na wasichana, hii ni kwa mujibu wa Kitokesya.