Na MOHAMED KASSARA
-DAR ES SALAAM
KOCHA msaidizi Mbao FC, Sudi Slim, amesema timu hiyo itafanya vizuri msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kuwa tayari ina uzoefu wa kutosha.
Mbao iliwashangaza wadau wa soka nchini baada ya kufika fainali ya Kombe la FA, lakini iliponea chupuchupu kushuka daraja ilipomaliza Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa kwenye nafasi ya 12.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Slim, alisema mazingira magumu waliyokutana nayo msimu uliopita yalitokana na ugeni wao, lakini anaamini msimu ujao watakuwa moto wa kuotea mbali.
“Ugeni ulitukwamisha kwenye ligi, tulipanda bila kutegemea, hivyo hatukuwa tunajua namna ya kukabiliana nao, lakini katika FA tulikuwa na uzoefu nayo ndio maana tulifikia hatua ya juu zaidi.
“Tutafanya vizuri msimu ujao kwa kuwa sasa tuna uzoefu, lakini pia tumesajili wachezaji wazuri kwa ajili ya kuziba mapengo ya wale walioondoka,” alisema Slim.
Mbao ilipanda daraja msimu wa 2015-16, baada ya timu za Geita Gold spot, Polisi Tabora na JKT Kanembwa kushushwa daraja kutokana na kashfa ya kupanga matokeo.