Na JANETH MUSHI
-ARUSHA
MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha, imelazimika kuwatafuta mawakili wa Serikali nje ya chumba cha mahakama wakati wa usikilizwaji wa rufaa ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), anayepinga uamuzi mdogo uliotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.
Uamuzi wa kuwatafuta walipo mawakili hao ulitokana na kutokuwapo kwao ndani ya chumba cha mahakama wakati shauri hilo likiendelea.
Kutokana na kukosekana kwa mawakili hao, Jaji Dk. Modester Opiyo, alilazimika kumwagiza Wakili wa Utetezi, Sheck Mfinanga, kutoka ndani ya chumba cha mahakama na kwenda kuwatafuta mawakili wa Serikali kwa sababu walitakiwa kuwa mahakamani hapo.
Kabla ya kutoa agizo hilo, Jaji Dk. Opiyo, alimtaka Wakili Mfinanga ampatie namba za simu za mawakili hao wa Serikali, Khalili Nuda na Innocent Njau, ambaye alisema hana namba za mawakili hao ingawa alikuwa ameuona Wakili Nuda nje ya mahakama hiyo kabla ya kesi kuendelea.
Kutokana na hali hiyo, Wakili Mfinanga alimuomba Jaji Opiyo apange tarehe nyingine kwa ajili ya kusikilizwa kwa rufaa hiyo kwa kuwa mawakili hao wa jamhuri hawakuwapo mahakamani
Hata hivyo, Jaji Dk. Opiyo alikataa ombi hilo na kumtaka wakili huyo wa Lema aende akawatafute mawakili hao nje.
“Nenda kawaite, mimi hainisaidii kitu chochote hii kesi kuendelea kukaa hapa kwani sipendi kukaa na kesi ya jinai kuanzia mwezi Machi hadi sasa bila kuendelea,”alisema jaji huyo na kumfanya wakili wa Lema akawatafute mawakili hao.
Wakihojiwa na Jaji Dk. Opiyo ni kwanini hawakuwa mahakamani wakati walitakiwa kuwapo, Wakili Nuda alisema yeye na mwenzake walifika mahakamani hapo kwa ajili ya kuendelea na kesi nyingine.
Kwa upande wake, Jaji Dk. Opiyo aliwaeleza mawakili hao, kuwa hiyo ni mara ya pili kwa mawakili wa Serikali kutofika katika shauri hilo ikiwamo Julai 12 mwaka huu kesi ilipoahirishwa baada ya wao kutofika mahakamani.
“Mara ya mwisho Wakili wa Serikali, Penina Joachim, alifika hapa rufaa ilipotajwa Mei mwaka huu, lakini leo ni mara pili kwa mawakili wa Serikali kutofika katika shauri hili,” alisema Jaji Dk. Opiyo.
Kutokana na hali hiyo, Jaji Dk. Opiyo alisema Septemba 27 mwaka huu, mahakama hiyo itapanga tarehe ya hukumu na kabla ya hukumu hiyo, Agosti 30, mwaka huu, mawakili wa Lema watawasilisha hoja zao ili zijibiwe na upande wa Jamhuri Septemba 13 na Septemba 20 hoja za ziada zitawasilishwa.
Katika rufaa hiyo namba 49 ya mwaka huu, Lema anapinga uamuzi mdogo uliotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, katika kesi ya kuhamasisha watu kukusanyika na kufanya maandamano ya Ukuta kinyume cha sheria.
Mawakili wanaomtetea mbunge huyo, waliwasilisha kwa njia ya mdomo taarifa ya kusudio la kukata rufaa Mahakama Kuu kupinga uamuzi huo uliotolewa Februari 8 mwaka huu, kwa kuwa wanataka kesi hiyo ikasikilizwe Mahakama ya Katiba mbele ya jopo la majaji watatu kutokana na kuwa na masuala ya kikatiba kwenye hati ya mashtaka.
Nashauri serikali iajiri mawakili kutoka nje ya nje (expatriates)kwani mawakili wake ni butu kupindukia. Inaonesha wakati mwingine hawajui watokako wala waendako!