30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Matola: Simba ni baba kwa Mtibwa Sugar

NA JESSCA NANGAWE-DAR ES SALAAM

KOCHA Msaidizi wa Simba, Seleman Matola, amesema licha ya ubora wa kikosi cha Mtibwa Sugar, wanachokwenda kupambana nacho, kwa upande wao wamejiandaa kupambana na kuibuka na ushindi na kutwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi.

Simba na Mtibwa Sugar, zitashuka dimbani kesho kuumana katika mchezo wa fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi, utakaochezwa Uwanja wa Amaan, Unguja.

Michuano hiyo ni maalum kwa ajili ya kuadhimisha Kumbukumbu ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika Januari 12, 1964 na kuuangusha utawala wa kisultan uliokuwa umeota mizizi visiwani humo.

Simba ilifanikiwa fainali ya Kombe la Mapinduzi, baada ya kuibuka na ushindi wa mikwaju ya penalti 3-2 dhidi ya Azam, katika mchezo wa nusu fainali uliochezwa juzi usiku Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Kabla ya mikwaju ya penalti kutumika kumsaka mshindi, timu hizo zilikamilisha dakika 90 kwa suluhu.

Kwa upande mwingine, Mtibwa Sugar ilifuzu nusu fainali baada ya kuiondosha Yanga kwa mikwaju 4-2, baada ya dakika 90 za mchezo huo kukamilika kwa sare ya bao 1-1.

Akizungumza na MTANZANIA, Matola alisema wanajivunia  historia nzuri wanapokutana na Mtibwa Sugar katika michuano mbalimbali, hivyo anaamini pamoja na ugumu wanaotarajia kukutana nao mwisho wa mchezo ubingwa utakuwa wao.

“Tuna historia nzuri ya kupata ushindi tunapokutana na Mtibwa, ni timu yenye ushindani lakini na sisi tunajipanga kukabiliana nayo na kushinda, tutapambana kuhakikisha ubingwa unakua wetu, hii itatusaidia pia kwenye ligi kuendeleza moto wa mapambano,”alisema Matola.

Simba ambayo ni bingwa mtetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ina rekodi ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi mara tatu.

Azam kwa sasa ndiye mfalme wa michuano hiyo, ikiwa imefanikiwa kutwaa taji la Mapinduzi mara tano tangu ilipoanzishwa rasmi mwaka 2007. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles