UINGEREZA,
MABILIONEA wanane wanamiliki utajiri ambao ni sawa na mali za watu bilioni 3.6 duniani kote.
Matajiri hao wanamiliki mali zenye thamani ya paundi za Uingereza bilioni 350 kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Oxfam nchini Uingereza.
Ripoti hiyo inaonesha matajiri hawa kwa pamoja wanautajiri wa jumla ya paundi bilioni 349.8 ambayo ni sawa na mali za nusu ya idadi ya watu ulimwenguni.
Tajiri namba moja wa dunia Bill Gates anaongoza katika orodha ya Shirika la Oxfam kwa utajiri wa paundi bilioni 61.6 akifuatiwa na Mhispania, Amancio Ortega bilioni 55 na mwekezaji Marekani, Warren Buffet, kwa utajiri wa bilioni 49.9.
Ripoti hiyo imetolewa kutokana na mkutano wa mwaka wa watu matajiri nchini Uswisi utakaowakutanisha wanasiasa, wakurugezi wa makampuni makubwa, mabenki, wanadiplomasia na watu maarufu.
Takwimu za shirika hilo, ambazo zimepingwa na baadhi ya wakosoaji, zinatokana na maelezo na habari za kina zilizokusanywa na shirika hilo na zinaonesha pengo kati ya matajiri na maskini ni kubwa kuliko ilivyodhaniwa awali.
Matajiri wengine ni Carlos Slim Helu wa Grupo Carso, paundi bilioni 41, Jeff Bezos, Amazon (bilioni 37.6) Mark Zuckerberg Facebook (bilioni 36.6, Larry Ellison, Oracle (bilioni 35.8) Michael Bloomberg, Bloomberg (bilioni 32.8).