30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mashine ya ultrasound yaibwa mazingira kutatanisha hospitali

Derick Milton -Simiyu

MASHINE inayotumika kupima magonjwa ya ndani na kutambua taarifa katika mwili wa binadamu (ultrasound), imeibwa katika mazingira ya kutatanisha Hospitali ya Mji wa Bariadi ya Somanda mkoani Simiyu.

Inadaiwa kuibwa na kifaa chake cha kudurufu picha (printer).

Mashine hiyo ambayo ilikuwa maalumu kwa matumizi ya wodi mpya ya wajawazito na iliibwa ikiwa katika wodi hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo, Mike Mabimbi, alisema mashine hiyo iliibwa Agosti 5 mchana, mwaka huu na hadi sasa haijapatikana.

Mabimbi alisema baada ya kutokea tukio hilo, walitoa taarifa polisi na watu 17 wakiwamo wauguzi walikamatwa kwa mahojiano.

“Ni kweli mashine hiyo ambayo ilitolewa na UNFPA kwa ajili ya wodi ya kina mama iliibwa katika mazingira ya kutatinisha, tayari taarifa tulitoa paolisi na wanaendelea na uchunguzi,” alisema Mabimbi.

Alisema mashine hiyo inafanana kama kompyuta mpakato (potable), hivyo mtu yeyote mwenye nia ovu alikuwa na uwezo wa kuiba na kuweka katika begi la mgongoni na kutoweka nayo.

“Mashine hiyo ilitolewa kwa ajili ya kina mama wajawazito tu na ilikuwa humo humo kwenye wodi kwa ajili ya kurahisisha huduma, na wodi hiyo ilikuwa na vifaa vyote vinavyohitajika kwa mama mjamzito kikiwemo chumba cha upasuaji,” alisema Mabimbi.

Alisema baada ya kuibwa kwa kifaa hicho, wanalazimika kuwapeleka kina mama wajawazito katika mashine kama hiyo kubwa iliyoko chumba cha mionzi, takribani mita 10 kutoka wodi yao na kueleza kuwa inasababisha usumbufu.

Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Mwanaidi Churu, alisema mazingira ya kuibwa kwa kifaa hicho yameendelea kuwa magumu kutokana na watoa huduma katika wodi hiyo waliokuwepo siku hiyo kila mmoja kudai hajui.

Alisema baada ya mashine hiyo kuibwa, wafanyakazi ambao walikuwapo zamu usiku hadi asubuhi waliitwa na walieleza kuwa kifaa walikiacha, na wale walioingia mchana walidai kutokikuta.

“Kila siku hapa hospitali ni vikao na bado kifaa hakijapatikana, ingawa huduma zinazendelea, ila kuna usumbufu kidogo maana kile kilikuwa humo humo ndani,” alisema Churu.

Hata hivyo, viongozi hao waliwaomba wananchi kutoa taarifa kwa polisi au kwa kiongozi wa Serikali yeyote endapo wataona kifaa kama hicho kinauzwa sehemu ili kiendelee kutoa huduma.

“Kifaa hiki kimeletwa hapa kutoa huduma kwa kina mama wajawazito, ambaye ameiba hakiwezi kumsaidia chochote, tunaomba waandishi wa habari na wananchi mtusaidie katika kupatikana kwa kifaa hiki, ni muhimu sana,” alisema Churu.

Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, William Mkonda kutaka kujua uchunguzi ulipofikia, hakuweza kupatikana na wasaidizi wake walieleza kuwa yupo katika kikao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles