24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 20, 2024

Contact us: [email protected]

Anayedaiwa kumuua mkewe kwa kumchoma moto, atishia kuwafanyia waandishi kitu kibaya

Kulwa Mzee -Dar es salaam

MFANYABIASHARA Hamis Said (38), anayedaiwa kumuua mkewe, Naomi Marijani kwa kumchoma na magunia mawili ya mkaa, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kwamba atawafanyia kitu kibaya waandishi wa habari ambacho mahakama haijakitarajia.

Mshtakiwa huyo alidai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi, Salum Ally, wakati kesi yake ya mauaji ilipokuwa ikitajwa kwa mara ya kwanza tangu alipofikishwa Julai 30, mwaka huu.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, akiiwakilisha Jamhuri, alidai kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi haujakamilika.

Wankyo baada ya kudai hayo, mshtakiwa Said alinyoosha kidole na kuomba aongee na mahakama iliruhusu.

“Mheshimiwa nina kitu ambacho nataka nikueleze kuhusu waandishi wa habari, wamekuwa wakinipiga picha kuanzia chini hadi ndani ya mahakama, sasa nakueleza hivi, nitakuja kuishangaza mahakama,  nitafanya kitu kibaya sana.

“Kuna kesi ambayo inanikabili na sielewi hatima ya kesi yangu, hapa nilipo kichwa changu kimevurugika, nina mawazo ya mtoto wangu na ninapofika hapa ili akili yangu itulie wanakuja kunipiga picha, sasa nawaeleza kuwa nitafanya kitu kibaya ambacho mahakama haitatarajia,” alidai.

Akijibu, Wakili Wankyo alimweleza mshtakiwa kuwa kupigwa picha ni hali ya kawaida na washtakiwa wote wanaofikishwa mahakamani wanapigwa picha, hivyo awape uhuru waandishi wa habari wafanye kazi yao kwa uhuru.

“Lengo la waandishi wa habari ni kutoa habari na kuwajuza wananchi, hivyo kumbuka hii ni mahakama na hatujui kitu unachotaka kufanya ni kitu gani,” alidai Wankyo.

Hakimu Ally baada ya kusikiliza hoja hizo, aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 27, kwa ajili ya kutajwa na mshtakiwa amerudishwa rumande.

Mtuhumiwa Said ameshtakiwa chini ya kifungu cha sheria namba 196 cha kanuni ya adhabu, sura ya 16 kilichofanyiwa marejeo mwaka 2002.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, anadaiwa alitenda kosa Mei 15, mwaka huu katika oneo la Gezaulole Kigamboni, Dar es Salaam ambako alimuua mtu anayeitwa Naomi Marijani.

Wakati akisomewa mashtaka, hakutakiwa kujibu kitu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles