SOCHI, URUSI
LICHA ya timu ya taifa ya Urusi kuondolewa katika michuano ya Kombe la Dunia nchini Urusi, mashabiki wa timu hiyo waliamua kutengeneza  vikundi kusafisha Uwanja wa Sochi, nchini humo.
Uamuzi huo ulifanywa baada ya kumalizika kwa mchezo wa robo fainali ambao Urusi iliondolewa kwa mikwaju ya penalti 3-4 dhidi ya Croatia zikimaliza dakika 90 zikifungana mabao 2-2.
“Hebu tukubali wenyewe kwamba usafi si kitu kipya kwetu. Lakini michuano ya Kombe la Dunia ni wakati mzuri wa kufanya jambo la tofauti na kuthibitisha kwamba sisi pia hatuwezi kuondoka tukaacha mlima wa takataka,” alisema shabiki mmoja aliyekuwa akizoa taka hizo.
Kitendo cha mashabiki hao kilionekana kuzua mjadala mkubwa katika mitandao ya kijamii, baada ya kuonekana wakiwa na mifuko wakizoa takataka.
Kitendo hicho ambacho pia kilifanywa na mashabiki wa timu ya taifa ya Japan na Senegal, kilionekana kuwagusa mashabiki wengi.