24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 20, 2024

Contact us: [email protected]

Mapya yaibuka mkoani Tanga

Na Amina Omari, TANGA
JESHI la Polisi nchini limesema katika msako unaoendelea katika mapango ya Mleni mkoani hapa, ambayo watu wanaodaiwa kuhusika katika matukio ya uporaji silaha walikuwa wamejificha, wamefanikiwa kukuta ngedere watatu wakiwa wamekufa huku wakiwa na majeraha.
Pamoja na hilo pia jeshi hilo limefanikiwa kumtia mbaroni mtuhumiwa mmoja ambaye wamemkuta na bunduki aina ya SMG ambayo ni mali ya jeshi hilo pamoja na risasi 20.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa Kamishana wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja, alisema wamefanikiwa kukamata silaha hiyo pamoja na mtuhumiwa mmoja anayedaiwa kuhusika katika tukio la uporaji wa silaha mbili mkoani hapa.
Alisema juzi walimtia mbaroni mtuhumiwa mmoja katika kona ya Z ambaye kwa sasa jina lake linahifadhiwa kwa sababu za kiusalama.
Chagonja alisema kukamatwa kwa mtuhumiwa kuyo kunatokana na taarifa zilizotolewa kwa jeshi hilo ambapo walikwenda kwenye eneo hilo na kufanikiwa kumkamata.
Alisema baada ya mahojiano ya kina, mtuhumiwa huyo aliweza kuwapeleka kwenye eneo la mapango ya Mleni na kufanikiwa kupata silaha hiyo ikiwa na risasi 20 ambayo baada ya kuichunguza ilibainika kuwa ni mojawapo iliyowahi kuporwa askari.
“Tunawaomba wananchi waepuke habari za pembeni, tumefanikiwa kufanya operesheni ya kina kwani hata tuliingia ndani ya mapango ya Mleni ambayo wahalifu walikuwa wamejificha, hatukukuta mhalifu yeyote zaidi ya ngedere watatu ambao walikuwa wamefariki wakiwa na majeraha.
“Kupatikana kwa silaha aina ya SMG yenye namba 14301230 ikiwa na risasi 20, ni juhudi kubwa za Jeshi la Polisi katika kuwezesha upatikanaji wa silaha zake zilizoibwa pamoja na silaha nyingine ambazo tunaweza kuzipata kwenye operesheni hii,” alisema Chagonja.
Kutokana na tukio hilo, Chagonja, aliwasihi wananchi waendelee kutoa taarifa kwa jeshi hilo ambazo zinasaidia kuwezesha kukamatwa kwa wahalifu pamoja na silaha ambazo bado hazijapatikana hadi sasa.
Hata hivyo, aliwataka Watanzania wawe na subira katika kipindi hiki ambacho jeshi hilo linaendelea na juhudi kuhakikisha watuhumiwa wote wanaofanya vitendo vya kihalifu ikiwamo uporaji wa silaha wanakamatwa.
“Ninawaomba wananchi waendelee kuviamini vyombo vya habari ambavyo vinatoa taarifa sahihi na achaneni na habari za uongo zinaoendelea kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii kwani hazina lengo zuri katika operesheni hii tunayoendelea nayo,” alisema Chagonja.
Alisema taarifa hizo zimekuwa zikiwachanganya wananchi na hata kuona hali ya usalama katika Mkoa wa Tanga si salama jambo ambalo si kweli kwani jeshi hilo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi wamefanikiwa kudhibiti hali ya usalama kwa raia na mali zao.
Juzi, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Juma Ndaki, alisema watu waliopambana na askari polisi na wale wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) ni kikundi cha wahuni.
Harakati za mapambano baina ya polisi na wahalifu hao zilidumu kwa takribani saa 48, huku Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Said Magalula, akikiri kwamba wameshindwa kuwakamata watu hao.
Ndaki aliwaambia waandishi wa habari kuwa jeshi hilo linawashikilia watu kadhaa kutokana na tukio la majambazi kushambuliana na askari polisi usiku wa kuamkia Jumamosi.
“Kuna watu kadhaa tumewakamata kuhusika na tukio hilo na upelelezi zaidi unaendelea ili kuweza kuwakamata wote waliohusika.
“Niwatoe hofu wananchi, tukio zima lilihusisha kikundi kidogo cha wahuni ambao walikuwa wanajificha katika mapango ya Kijiji cha Mleni kwa ajili ya kufanya shughuli za kiuhalifu,” alisema Ndaki.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Magalula, alisema hali katika mji wa Amboni ni salama na kuwa waliokuwa wanapambana na polisi ni majambazi na si magaidi.
Magalula alisema mapambano hayo yalilenga kuwapata wahalifu ambao walipora silaha za polisi mwishoni mwa Januari.
Katika siku ya kwanza ya operesheni hiyo, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na JWTZ walipiga mabomu ya machozi kwenye mapango walimojificha wahalifu hao katika harakati za kuwakamata, hali inayoweza kuwa chanzo cha vifo vya ngedere waliokutwa juzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles