23.7 C
Dar es Salaam
Thursday, September 28, 2023

Contact us: [email protected]

Akamatwa akidaiwa kuuza nyama ya paka

Na Asifiwe George na Mwantum Saadi, Dar es Salaam
MUUZA mishikaki mmoja katika kituo cha daladala cha Temeke mwisho jijini Dar es Salaam maarufu kwa jina la Said Mishikaki, amekamatwa na kupigwa na wananchi kwa tuhuma za kuuza mishikaki ya nyama ya paka.
Said alikamatwa jana asubuhi baada ya taarifa kusambaa katika eneo hilo zikimtuhumu kwamba amekuwa na kawaida kuuza mishikaki ya nyama ya paka badala ya ng’ombe, mbuzi na wanyama wengine wanaoliwa.
Taarifa zilizopatikana kutoka eneo la tukio zinasema kuwa, baada ya taarifa hizo kuenea, wananchi walilazimika kumtafuta muuza mishikaki huyo ili wamchukulie hatua.
Baada ya kumsaka kwa dakika kadhaa, hatimaye walifanikiwa kumkamata na kumkuta akiwa na paka mmoja aliyekuwa amemchinja na kumuweka kwenye ndoo.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, wananchi hao walipomuona paka huyo akiwa amechinjwa, walichachamaa na kuanza kumshushia kipigo muuza mishikaki huyo na kumuumiza sehemu mbalimbali za mwili wake.
Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Kihenya Kihenya, alipozungumza na MTANZANIA kwa simu, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Hata hivyo, alisema taarifa za tukio hilo zinahitaji uchunguzi zaidi ili kuzithibitisha.
“Nilikwenda eneo la tukio na kukuta kielelezo cha mfuko wa nyama hiyo. Niliona nyama na utumbo mkubwa unaoonekana kama ni wa mnyama anayekula majani mfano wa ng’ombe.
“Inawezekana kuna matatizo katika biashara, huenda kweli ile ilikuwa nyama ya paka, lakini hatuna uhakika, hivyo tumechukua vipande vya nyama kwa ajili ya kuvipeleka kwa mtaalamu wa mifugo kwa uchunguzi zaidi ili kubaini aina hiyo ya nyama.
“Nyama hizo zilikuwa zinaonekana kubwa kama nyama za kuchemsha na utumbo ni mkubwa kama wa ng’ombe. Mimi nimeona haielekei kuwa ni ya paka. Kwa ujumla, hili jambo linahitaji uchunguzi zaidi,” alisema Kamanda Kihenya.
Pamoja na hayo, Kamanda Kihenya alionyesha kutoridhishwa kitendo cha wananchi hao kumpiga muuza mishikaki huyo.
Alisema wananchi hao walitakiwa kutoa taarifa katika vyombo vya dola badala ya kujichukulia hatua mkononi.
Akizungumzia ulaji wa nyama ya paka, mmoja wa madaktari bingwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. David Kombo alisema haina madhara yoyote kwa binadamu.
“Nyama ya paka haina madhara yoyote ya kiafya kwa binadamu, yaani binadamu hawezi kudhurika kwa kula nyama hiyo labda tu mnyama huyo awe na maradhi fulani fulani .
“Kwa kuwa nyama hiyo hailiwi katika mazingira yetu, baadhi ya watu wanapotambua wameila, wanaanza kujisikia vibaya kwa kuwa si kitu cha kawaida katika utamaduni wetu.
“Lakini, ikumbukwe kwamba baadhi ya nchi za Mashariki ya Mbali kama China na Korea, wanakula nyama ya aina yoyote ikiwamo paka, nyoka, mbwa na wanyama wengine ambao kwa utamaduni wetu ni jambo la ajabu.
“Pamoja na kwamba watu hao wanakula wanyama hao tusiowala sisi, hawapati madhara yoyote, kwa hiyo hakuna tatizo,” alisema Dk. Kombo.
Tukio hilo na mishikaki ya paka linafanana na tukio jingine la aina hiyo lilitokea mjini Mbeya Novemba 4, mwaka jana ambapo Jeshi la Polisi mkoani humo, lilimkamata muuza mishikaki mmoja, Ahadi Jesikaka (20), mkazi wa Kijiji cha Ngyekye kwa kosa la kuwauzia watu nyama ya mbwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,745FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles