26.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Mapambano corona Uamuzi kusitisha ibada Katoliki waachiwa maaskofu

WAANDISHI WETU-DAR/DODOMA

KANISA Katoliki limesema maaskofu wa majimbo husika ndio wenye mamlaka ya kusitisha ibada za misa na maadhimisho mengine iwapo wataona inafaa ili kujihadhari na maambukizi ya virusi vya corona.  

Kutokana na virusi vya corona kuendelea kuenea maeneo mbalimbali nchini, ushauri umekuwa ukitolewa kwa viongozi wa dini kusitisha ibada, lakini ni wachache waliotekeleza.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Rais wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Gervas Nyaisonga, alisema kila askofu ana mamlaka kwenye jimbo lake, ingawa kuna baadhi ya mambo wanayafanya kwa ushirikiano.

“Kila askofu ana mamlaka kwenye jimbo lake, ndiyo utaratibu, ni tofauti na mifumo mingine. Kuna mengine kila askofu anaweza akatafsiri kanuni zile tulizoweka za jumla akazitekeleza kwenye jimbo lake na ndiyo maana yeye (Askofu Severine Niwemugizi) amefanya hivyo.

“Wengine tunaamini zaidi miongozo inayotolewa na Serikali, wengine wanaamua kuongeza zaidi kupita yale ambayo Serikali imetoa, kwa hiyo, hiyo inawezekana katika mazingira yoyote.

“Kuna mtu anaweza akaamua yeye kuongeza au mwingine akasema naamini Serikali ina nia njema, imeelekeza hivi anafuata yale ambayo yameelekezwa na Serikali, lakini hakuna lililoharibika katika mahusiano ya kawaida,” alisema Askofu Nyaisonga.

Alisema wanafanya kazi zao kwa kuheshimu mamlaka ya kila mtu kwenye nafasi yake na kwamba wao ambao wamepewa nafasi ya uongozi wanasimamia yale ambayo wamekubaliana ndani ya umoja wao.

KKKT

MTANZANIA lilimtafuta Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Frederick Shoo, ili kupata msimamo wao lakini simu yake haikupatikana.

Alipotafutwa Katibu Mkuu wa KKKT, Brighton Killewa, alisema masuala yote yahusuyo kanisa msemaji mkuu ni Dk. Shoo.

RULENGE/KARAGWE

Tayari maaskofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge – Ngara na KKKT Dayosisi ya Karagwe mkoani Kagera wametangaza kusitisha ibada kuepuka kuenea kwa virusi vya corona katika maeneo yao.

Katika Jimbo Katoliki la Rulenge – Ngara ibada za misa, maadhimisho mengine yanayokusanya waumini wengi kanisani na sala za jumuiya zimesitishwa kwa mwezi mmoja kuanzia Aprili 19 wakati Dayosisi ya Karagwe zitasitishwa kuanzia Aprili 26.

Askofu wa Jimbo la Rulenge, Severine Niwemugizi, alisema baada ya muda uliopangwa kumalizika, wataangalia hali itakavyokuwa na ikibidi muda wa kusitisha ibada utaongezwa.

“Baada ya kutafakari alama za nyakati na kujifunza kutoka kwa wenzetu Ulaya na Marekani, nchi jirani zetu na hatua ambazo Baba Mtakatifu alizichukua kwa kutoa maelekezo kwa maaskofu wa Katoliki duniani namna ya kuadhimisha ibada katika kipindi hiki cha vita dhidi ya corona, nimebeba dhamana ya kutoa uamuzi mgumu.

“Tutaomba Redio Kwizera irushe adhimisho la misa fupi ili waumini wafuatilie redioni na baada ya muda huo kumalizika tutaona hali itakuwaje na ikibidi tuongeze muda tutafanya hivyo,” alisema Askofu Niwemugizi.

Aliwataka mapadri kuadhimisha misa peke yao kwa niaba ya waumini kuwaombea na kuiombea dunia ili Mungu anusuru janga hilo na kuagiza sala za jumuiya kufanyika ndani ya familia kwa familia moja moja.

Katika Dayosisi ya Karagwe, Askofu Dk. Benson Bagonza alitangaza kusitisha ibada zote kuanzia Aprili 26 akitaja sababu zilizofanya afikie maumizi hayo kuwa ni pamoja na dayosisi hiyo kuwa mpakani na nchi ambazo raia wake wanatoroka na kuingia nchini.

MAJALIWA KUONGOZA MAOMBI

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, leo anatarajiwa kuongoza maombi ya kitaifa kuiombea nchi dhidi ya maambukizi ya corona yatakayofanyika katika viwanja vya Karimjee.

Maombi hayo ambayo ni mwendelezo wa maombi ya siku tatu mfululizo yaliyotangazwa na Rais Dk. John Magufuli yameandaliwa kwa ushirikiano na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini.

Taarifa iliyotolewa jana na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Afya – Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Prudence Costantine, ilisema viongozi wachache watahudhuria maombi hayo kuwakilisha wananchi.

“Hatua hii ni utekelezaji wa maazimio ya mkutano wa viongozi wa dini na Serikali uliofanyika Aprili 9 mwaka huu, kuwa wafanye maombi ya kitaifa yanayojumisha madhehebu yote nchini.

“Viongozi wachache watahudhuria maombi haya kuwakilisha wananchi ikiwa ni katika hali ya kuchukua tahadhari ya maambukizi, hivyo wananchi wanaendelea kusisitizwa kuchukua tahadhari dhidi ya corona na kufuatilia maombi haya mkiwa katika maeneo yenu kupitia vyombo mbalimbali vya habari,” alisema Costantine.

NDUGAI AWAONDOA HOFU WABUNGE

Licha ya corona kuingia bungeni, Spika Job Ndugai pia alisema shughuli za Bunge hazitasitishwa na badala yake kazi zilizopangwa zitamalizika kwa wakati.

Alisema kama kuna mbunge anajisikia vibaya au kuona dalili zilizotajwa, atoe taarifa na kujiweka mwenyewe karantini na kuhusu utaratibu mwingine asijali.

Kauli hiyo aliitoa bungeni jana wakati akijibu mwongozo wa Mbunge wa Nsimbo, Richard Mbogo (CCM), ambaye aliitaka Serikali ichukue hatua kuwapima corona wabunge na wafanyakazi wote.

Akijibu mwongozo huo, Ndugai aliwataka wabunge kuendelea kuchukua hatua wenyewe na kuwahakikishia watabaki salama hususani kipindi hiki cha corona.

Alisema si kila mtu anaishi hapo saa 24 kwa kuwa haiwezekani kuwadhibiti wabunge au wafanyakazi wote, hususani watu wanaokutana au kuchanganyika nao nje.

“Ni kweli tumeanza kuguswa maana ni sehemu ya jamii haiwezekani tusiguswe, tundelee kujipa moyo ili tusonge mbele kumaliza kazi hii.

“Kazi yetu tutamalizia hata kama ni kwa muda mfupi, mawazo ya kwamba kazi hii italala hakuna, Ndugai akiwa hayupo atakuwepo mwingine,” alisema Ndugai.

Aliitaka Serikali kutenga nafasi siku za Bunge ili kuja kueleza kwa kirefu suala la ugonjwa huo na kushauri kuwa katika maeneo mengine iundwe kamati ya ufuatiliaji na mara kwa mara taarifa itolewe.

HALI ILIVYO

Takwimu zilizotolewa juzi na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, zilionyesha kuwepo kwa wagonjwa wapya 84 huku 16 wakitolewa taarifa Zanzibar.

Hivyo, idadi ya wagonjwa imeongezeka kutoka 170 hadi 254 huku vifo vikifikia 10 baada ya vitatu kuripotiwa juzi.

Kwa upande wa Tanzania Bara, idadi ya wagonjwa na mikoa wanakotoka ni Dar es Salaam (33), Arusha (4), Mbeya (3), Kilimanjaro (3), Pwani (2), Tanga (3), Manyara (2), Tabora (1), Dodoma (3), Ruvuma (2), Morogoro (2), Lindi (1), Mara (1), Mwanza (3), Mtwara (1), Kagera (1) na Rukwa (2).

HABARI HII IMEANDALIWA NA NORA DAMIAN NA AVELINE KITOMARY (DAR) NA RAMADHAN HASSAN (DODOMA)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles